Tuesday, August 20

Kiwanda cha alizeti kujengwa Z’bar

0


Na Othaman Khamis,OMPR

Katika kuhakikisha kasi ya uanzishwaji na ukuaji wa viwanda unaimarika Zanzibar shirika la kimataifa linalojishughulisha na uzalishaji wa kilimo cha alizeti la Alemdar Uturuki, limeonyesha nia ya kutaka kujenga kiwanda kitakachozalisha bidhaa tofauti kwa kutumia malighafi ya maua hayo katika azma ya kuitikia wito wa serikali wa kuwa nchi ya viwanda katika kipindi kifupi kijacho.

Hayo yamebainika baada ya ofisa Mkuu wa shirika hilo, Fatma Atala, alieleza hayo wakati ujumbe wa viongozi wa shirika hilo ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Oktay Alemder, ulipokutana kwa mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Vuga mjini Zanzibar.

Alisema mradi huo wa kibiashara endapo utafanikiwa kuanzishwa unalenga pia kuwashirikisha moja kwa moja wakulima vijijini kwa kulima maua ya alizeti katika baadhi ya maeneo yao ya kilimo.

Alisema maua ya alizeti ni bidhaa inayoendelea kuwa na hadhi kubwa katika masoko ya kimataifa ambayo inaweza kusaidia kunyanyua mapato ya washiriki katika ukulima wake sambamba na kuongeza mapato ya taifa.

Akitoa shukrani zake, Balozi Seif aliueleza ujumbe huo wa viongozi hao kwamba Tanzania tayari imeamua kuwa nchi ya viwanda ifikapo 2025.

Alisema wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wana fursa ya kuitumia nafasi hiyo katika ushiriki wao wa uwekezaji utakaokwenda sambamba na azma hiyo ya serikali.

Hata hivyo, alifahamisha kwamba ujumbe huo unapaswa kuzingatia zaidi mazingira halisi ya zanzibar yanayoendelea kukumbwa na changamoto ya ufinyu wa ardhi.

Aliushauri ujumbe wa viongozi hao kutayarisha maombi na kuyawasilisha kwa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) kwa hatua ya kuangalia uwezekano wa kuufanyia uchambuzi yakinifu mradi wao na mazingira halisi ya ardhi yaliyopo Zanzibar.

Aliuhakikishia Ujumbe huo wa Viongozi wa shirika hilo  kwamba serikali iko tayari muda wowote kuunga mkono jitihada za shirika hilo za kutaka kuitumia fursa ya uwekezaji vitega uchumi iliyopo Tanzania.

 

Imehaririwa na Mohamed Khamis

Share.

About Author

Leave A Reply