Tuesday, July 23

Zungu atoa sababu wafanyabiashara kuikimbia Tanzania

0


Dodoma. Mbunge wa Ilala (CCM) Mussa Zungu amesema wafanyabiashara wamekimbia nchini Tanzania kutokana na kukosekana kwa mazingira rafiki katika masuala ya kodi na ushuru.

Zungu ameyasema hayo bungeni leo Alhamisi Novemba 8, 2018, wakati akichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20.

Amesema bishara katika maeneo ya bandari na maeneo mengine si rafiki kwa wasafirishaji na waingizaji wa bidhaa nchini.

Amesema gharama ya kontena la futi 20 katika Bandari ya Kenya ni Dola za Kimarekani 80 ambayo wamepunguza kutoka Dola za Marekani 103.

Hata hivyo, amesema kwa Tanzania kontena lenye ukubwa huo gharama zake ni Dola za Marekani 170 ni vigumu kwa waingizaji wa bidhaa kuvutiwa kuitumia.

Amesema katika Bandari ya Dar es Salaam inayotegemewa  ‘handling charge’ kwa usafirishaji ni Dola za Marekani 100 lakini Kenya ni Dola za Marekani 60.

“Utakuta lazima watu wengi wanahamia katika bandari yenye unafuu, namuomba waziri aendelee kuchagua ushauri wa namna gani anaweza kupunguza tariff (kodi) na kodi za ‘importation’ ishuke ziwe rafiki kwa wafanyabiashara,” amesema.

Aidha, ameitaka Serikali kutazama gharama za kodi na kwamba wakati wanaanza kutoza VAT walianza na kiwango cha asilimia 20 lakini ikaendelea kupungua hadi kufikia 18.

Amesema uzalishaji wa vinywaji baridi umeshuka kwa sababu gharama ni kubwa na Watanzania hawawezi kumudu kununua.

Amesema ukipunguza kodi uzalishaji utakuwa mkubwa na kwamba Serikali haitapoteza kodi bali itaongeza.

Zungu amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango kutazama gharama za uingizaji wa sukari ya viwandani na kwamba wawekezaji wanalalamika hawajarudishiwa fedha walizoweka kama deposit kwa miaka mitatu.

“Sasa zimefika zaidi ya Sh45bilioni na hii ni mitaji ya wafanyabiashara na wanalipa kodi vizuri. Serikali ikitazama maeneo ya kushirikiana nayo mapato mengi ya kodi itayapata. Viwango vikubwa vya kodi tunavyoviweka vinawakimbiza wafanyabiashara,” amesema.

Amesema wafanyabiashara wengi wanakimbilia nchi nyingine na kuomba kuwa na utaratibu mzuri wa kodi ambao utawavutia wafanyabiashara wengi nchini.

Share.

About Author

Leave A Reply