Wednesday, August 21

Wizara ya Sheria na Katiba yasema ndoa kwa wahanga wa udhalilishaji husababisha kesi za udhalilishaji kutomalizika

0


By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Kitendo cha kufungishwa ndoa wanawake waliofanyiwa vitendo vya udhalilishaji kabla ya kesi zao kumalizika mahakamani, kimedaiwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia kutomalizika kwa matukio ya udhalilishaji ya wanawake visiwani hapa.

Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Khamis Juma Maalim ameyasema hayo leo Alhamis Mei 30, 2019 katika mkutano wa baraza la wawakilishi huko Chukwani, nje kidogo ya mji wa Unguja, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Konde, Omar Seif Abeid.

Katika swali lake,  Abeid alitaja kujua kutokana na uwapo wa wingi wa kesi Mahakamani hasa za udhalilishaji Mahakama zina mpango gani wa kupanga siku maalumu kwa ajili ya kuzisikiliza kesi hizo ili kuziharakisha hali ambayo pia itasaidia kupunguza msongamano wa kesi kama hizo.

Akijibu swali hilo, Waziri Juma alisema licha ya Mahakama kufanya jitihada za kuzishughulikia kesi hizo, lakini kitendo cha wanafamilia hasa upande wa kikeni kuamua watoto wao waliofanyiwa udhalilishaji kuwafungisha ndoa na wahusika kunasababisha kesi nyingi kutopatiwa ufumbuzi.

Alisema kuna baadhi ya wanafamilia hata kesi ikiwa katika ngazi za Mahakama, nao huamua kupitisha suluhu baina yao na familia ya watendaji wa matukio hayo na baadhi yao huafikiana kuwafungisha ndoa watoto wao.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema  kuanzia Julai 2018 hadi Machi 2019, kesi 16 tu za udhalilishaji zilikuwa zimesikilizwa na kutolewa hukumu na kati ya kesi hizo, 13 washtakiwa wametiwa hatiani na kesi tatu washatakiwa wameachiwa huru.

Waziri Juma alisema katika kipindi hicho pia kuna kesi 251 zinazosikilizwa katika hatua mbalimbali na kesi saba kati ya hizo zimefikia hatua ya wahusika kutoa utetezi, kesi tisa hatua ya uamuzi mdogo na kesi 235 zinasikilizwa.

Share.

About Author

Leave A Reply