Friday, July 19

Waziri Mkuu mgeni rasmi siku ya Ukimwi

0


Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ukimwi duniani yatakayofanyika mkoani hapa Desemba Mosi mwaka huu.

Akizungumza leo Novemba 21 2018, Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Stella Ikupa amesema maadhimisho hayo yataanza Novemba 24 na kilele chake ni Desemba Mosi.

“Kauli mbiu ya maadhimisho haya mwaka huu ni Pima, Jitambue, Ishi. Kauli mbiu hii inalenga katika kutoa msukumo wa upimaji wa hiyari wa Virusi vya Ukimwi (VVU) baada ya ushauri nasaha pamoja na kuanza kutumia dawa (ARV) mapema baada ya kugundulika na maambukizi ya VVU,”amesema.

Amesema matukio mbalimbali yatafanyika katika kuadhimisha siku hiyo ikiwemo huduma nyingine za afya hasa za magonjwa sugu yasiyoambukiza.

Amesema mwaka huu maadhimisho hayo yametoa kipaumbele kwa vijana kwa sababu wanatambua kuwa wanakabiliwa na changamoto nyingi na takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya maambukizo mapya ya VVU kutokea kwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24.

Amesema katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa kutakuwa na sehemu maalum ya mabanda itakayojulikana kama kijiji cha vijana.

Amesema kwa kushirikiana na wasanii maarufu nchini ujumbe mbalimbali utatolewa kwa njia ya kufikisha elimu ya VVU na Ukimwi kwa vijana wa vyuo, shule za sekondari na msingi pamoja na vijana walio nje ya shule.

Stella amesema katika kijiji hicho pia itatolewa elimu ya stadi za maisha, upimaji kansa ya shingo ya uzazi na elimu ya uchoraji pamoja na ujasiriamali.

“Nachukua fursa hii kuwakaribisha wananchi wa Dodoma na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kuja kupata huduma hizo za watu wote na zile zinazolenga vijana na zitatolewa bure,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply