Tuesday, August 20

Watatu mbaroni wakituhumiwa kuuza mizoga ya ng’ombe wenye kimeta

0


By Lilian Lucas, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Watu watatu wanashikiliwa na Polisi Mkoani Morogoro kwa tuhuma za kukutwa wakiuza nyama ilitokana na mizogo ya ng’ombe walioumwa kimeta.

Wanadaiwa mizogo hiyo ilikuwa imefukiwa wakaifukua.

Kamanda wa Polisi Mkoani Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema hayo leo Jumatano Mei 22, 2019, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa  tukio la kukamatwa watuhumiwa hao lilitokea Mei 18 saa 8.30 mchana katika Kijiji cha Pangawe, Kata ya Mkambarani.

Mutafungwa amesema watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na mizoga ya ng’ombe saba ambao walikufa kwa kimeta baada ya kuthibitishwa na daktari wa mifugo, Michael Sule.

Amesema ng’ombe hao walikuwa wakimilikiwa na mfugaji Dickson Msurwa mkazi wa Nane nane, baada ya kufukiwa waliifukua na kuanza kuwauzia watu mitaani.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Salum Lukanda aliyekamatwa na mapaja mawili ya ng’ombe nyumbani kwake akiwa na mwenzake na walikutwa wakiiuza nyama hiyo maeneo ya Kingolwira.

Amesema polisi walipata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Pangawe, Matata Ndida, ndipo walianza msako kufanikiwa kuwakamata Matata Shija (53) na Joseph Mhagama Makono (17), wote wakazi wa Pangawe, ambao nao walikutwa wakiuza nyama hiyo.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi kuepuka kujitafutia kipato kwa njia isiyo halali, kwa kufanya hivyo kunahatarisha maisha ya wengine, ugonjwa huu wa kimeta ni hatari,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Ofisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Morogoro, Mohamed Chamzhim akizungumzia suala la kimeta amesema baada ya kupata taarifa kuuzwa kwa nyama hiyo yenye kimeta, walilazimika kufanya  msako kwenye bucha zilizoko maeneo ya Kingolwira na walifanikiwa kufunga bucha mbili zilizokutwa zikiuza nyama hiyo.

Chamzhim amesema kama idara ya mifugo, wameendelea kutoa tahadhari kwa wauzaji na wenye bucha kuacha kununua nyama ambayo haijapimwa.

Amesema kwa kushirikiana na umoja wa wafanyabiashara wa nyama (Uwamo) wanaendelea kufanya ukaguzi.

“Tunatoa elimu kwa wananchi kutoendelea kukubali kupewa ama kununua nyama mbayo haijakaguliwa na wanapoona watu wanauza, watoe taarifa haraka,” amesema ofisa huyo wa mifugo.

Amesema katika ukaguzi huo, walifanikiwa kukamata kilogram 18.3 za nyama, ini moja na bandama moja kwenye bucha za Emanuel Chitema na mmoja wa waliohusika na uuzaji wa nyama hiyo ya mzoga Hassan Maganga alikimbia baada ya kuwaona askari na maafisa mifugo.

Share.

About Author

Leave A Reply