Monday, August 26

Watanzania wanaoishi nje ya nchi waombewa kupiga kura

0


By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema suala la Watanzania waishio nje ya nchi ni la kisera zaidi Serikali itakapojiridhisha wanaweza kuruhusiwa kupiga kura katika chaguzi.

Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 23,2019  katika kipindi cha maswali ya hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Adha Abdul Juma aliyehoji kama Watanzania waishio nje ya nchi wanaweza kupata nafasi ya kupiga kura wakati wa uchaguzi.

Mbunge huyo amehoji ni lini Watanzania  hao wataruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi kama wanavyofanya mataifa mengine.

“Serikali yetu imefanya kazi kubwa kusimamia Ilani ya uchaguzi ya CCM,  ikiwa ni pamoja na suala demokrasia, hivyo tunahitaji kuwatambua wenzetu wanaoishi nje,  ni lini nao hao wataruhusiwa kupiga kura,” amehoji Juma.

Katika maelezo yake zaidi Majaliwa amesema ili kuruhusu watu hao kuwa na haki ya kupiga kura ni lazima kujua nani yupo nje ya nchi na anafanya kazi gani au kama amebadili uraia wake au bado ni Mtanzania.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu ameliambia Bunge kuwa taarifa ya kamati ya mawaziri iliyoundwa kuchunguza migogoro ya ardhi ni mali ya Rais John Magufuli hivyo haiwezi kupelekwa bungeni bila idhini ya mwenye kamati.

Mbunge Nsimbo (CCM),   Richard Mbogo ametaka serikali kuruhusu ripoti ya mawaziri wanane iliyokuwa chini ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ipelekwe bungeni kabla ya kwenda kwa Rais ili waangalie dosari na upungufu.

Share.

About Author

Leave A Reply