Thursday, August 22

Wataalamu mipango miji wampinga Lukuvi urasimishaji viwanja

0


By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Wataalamu wa Mipango Miji (TAP) kimepinga punguzo la bei ya kurasimisha viwanja iliyotangazwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na kimesema kinatafakari hatua zaidi ya kuchukua.

Lukuvi alitangaza kushusha bei hiyo jana Jumatano jijini Dar es Salaam kutoka Sh250,000 ya awali hadi Sh150,000, akisema imelenga kuwapunguzia mzigo wananchi ili waweze kulipa kodi kupitia viwanja vyao.

Alisema lengo ni kufikisha viwanja 500,000 vitakavyokusanya kodi ya Sh24 bilioni kwa miezi mitatu.

Lakini akizungumza leo Alhamisi Aprili 18, 2019, msemaji wa TAP, Dk Juma Matindana amesema hawakushirikishwa katika kupanga bei hiyo.

“Kilichofanyika jana ni waziri kutoa maelekezo ya bei na siyo mapendekezo ili tujadili. sasa kwenye practice (utendaji) hicho kitu hakipo. Ni sawa na wizara ya afya iseme kupima malaria ni Sh1,000 au sukari unaweza kuipangia bei, lakini huwezi kumpangia mtoa huduma bei, kwa sababu sisi tunatoa huduma siyo bidhaa.”

“Mtaalamu akienda ‘field’ posho yake ni tofauti na graduate (mhitimu wa shahada), ni tofauti na mwenye diploma,” amesema.

Amesema kampuni zinazofanya urasimishaji wa makazi zimesajiliwa na zinalipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), hivyo bei iliyotangazwa na waziri huyo haieleweki kama tayari imekatwa kodi au bado.

“Kesho tutafanya kikao kutathmini hii bei, kwa kweli ni uonevu, haiko sawa,” amesema Dk Matindana.

Mtaalamu mwingine ambaye aliomba jina lake lisitajwe licha ya kusema hawakushirikishwa kupanga bei, amesema Lukuvi aliangalia upande mmoja tu wa kampuni bila kuangalia ucheleweshaji wa malipo kutoka kwa wananchi.

“Kwanza wananchi wanatakiwa watoe asilimia 30 ya kuanzia kwa utambulisho, kisha baada ya hapo wanatoa tena asilimia 30 ya michoro na malipo ya mwisho baada ya kazi. sasa utakuta hadi mnamaliza kati ya watu 100 waliotoa ni 10 tu, utamalizaje kazi?” alihoji mtaalamu huyo na kuongeza:

 “Kuna mambo mengi ya kulipia, kwa mfano kuna vifaa vinakodishwa na vikikaa sana gharama zinaongezeka, magari yanataka mafuta, kuna vijana wa kufanya kazi, kuna mtu anayetoka kamati ya wananchi naye analipwa, kuna kodi za kulipa manispaa na bado unatakiwa ukodishe ofisi, wananchi waione. angalau Sh250,000 ilikuwa inatosha.”

Share.

About Author

Leave A Reply