Tuesday, August 20

Wapinzani waibua sakata la balozi EU kuondoka Tanzania

0


By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka Serikali kulieleza Bunge sababu za kumuwekea shinikizo aliyekuwa balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Roeland van de Geer na kusababisha kurejea kwao.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Mei 30, 2019 na Salome Makamba aliyekuwa akisoma taarifa ya kambi hiyo kwa niaba ya msemaji wa upinzani wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano  wa Afrika Mashariki, Esther Matiko.

Salome amesema hakuna Serikali duniani inayoweza kufanikiwa bila kuwa na uhusiano na mataifa mengine, kwamba ni bahati mbaya Tanzania  inagombana mpaka na wahisani wanaoipatia misaada ya bajeti.

“Kambi inapenda kujua ni kwa nini Serikali imeanza kuwa na tabia ya kuziingilia na kuziwekea mashinikizo Balozi zinazoziwakilisha nchi zao katika utendaji wa kazi ikiwa haziendi kinyume na mkataba wa Vienna.”

“Hata kama Serikali inaona Balozi hizo zinakiuka mkataba wa Vienna katika utendaji wao wa kazi,  Bunge linapaswa kuelezwa ni mambo gani Balozi hizo zinafanya mpaka kustahili shinikizo,” amesema Salome.

Ameongeza, “Mpaka sasa Jumuiya ya Ulaya ambayo imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya Tanzania katika sekta mbalimbali haina ubalozi nchini.

Amesema kutikisika kwa uhusiano baina ya Tanzania na EU hauwaathiri viongozi wa CCM pekee, bali wananchi wanaonufaika na misaada ya jumuiya.

Amesema kambi hiyo ya upinzani inaishukuru Jumuiya ya Kimataifa hususan Umoja wa Ulaya na ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa kuendelea kupaza sauti dhidi ya vitendo viovu vya ukandamizaji wa demokrasia na haki za binadamu.

“Mungu atawalipa kwa kazi kubwa mnayofanya ya kuhakikisha uhai, uhuru na utu wa mwanadamu vinalindwa na kuheshimiwa duniani kote,” amesema Salome.

Share.

About Author

Leave A Reply