Sunday, August 25

Wananchi wahoji uhalali wa fedha za marehemu kwenda BOT

0


By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Wananchi mbalimbali wamehoji uhalali wa fedha za mtu aliyekufa ambazo zilihifadhiwa katika huduma za fedha kupitia simu ya mkononi na benki, kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BOT)  ilhali marehemu alikuwa na ndugu na wategemezi.

Hayo yameibuka baada ya gazeti la Mwananchi la leo Aprili 29, 2019 kuandika ripoti maalumu iliyoangazia mtiririko wa fedha za mtu aliyefariki dunia au kupatwa na majanga mengine namna amana zao zinavyokusanywa na kufikishwa mahala husika kupitia sheria ya mali isiyo na mwenyewe (Unclaimed Property Act).

Wasomaji mbalimbali wametoa maoni yao kupitia mitandao ya kijamii ya Mwananchi ya Facebook na Twitter kuhusu sakata hilo, wakitaka mabadiliko yafanywe na fedha hizo kutangazwa ili ndugu wajitokeze kupitia mahakama na  warithi wapate urithi wao.

Habibu Goatee amesema, “Ilishatokea sikutumia laini yangu kwa zaidi ya miezi sita wakaifungia na pesa zake lakini nilipofuatilia nilirudishiwa na pesa yote ikiwemo, ingawa nilipata shida ikiwemo kutoa gharama kubwa ili ifunguliwe tena.”

Hata hivyo Joseph Madeleine amesema suala hilo bado linashusha uaminifu kati ya mitandao ya simu, mabenki na fedha zinakotakiwa kupelekwa yaani BOT.

“Hapa sasa ndio kwenye uaminifu kati ya mtandao husika na TCRA na benki B O T, nina wasiwasi na hawa wa mitandao laini zinazoripotiwa TCRA ni zile zenye hela ndogo ndogo 2,000, 500 lakini za kuanzia 10,000 hawazioni BOT,” amesema.

Abdallah Mikulu amesema, “habari nzuri sana na imeelewesha watu, kama baada ya miaka 15 ndiyo Serikali huzitumia, basi imani yangu ni kwamba basi toka huduma hizi za  pesa zianze haijapita miaka 15. Hivyo kwa zile familia zilizopoteza  wenza wao au ndugu zao wanao muda  wa kufuatilia kwani Watanzania wengi tulikuwa hatujui utaratibu huu.”

Ameongeza kuwa kwa nia njema BOT sasa wangechapisha majina tu ya watu ambao hazina zao zilishawasilishwa kule na baada ya hapo utaratibu uendelee kwani kuna majanga mengi yamepoteza wengi tena wengine wafanyabiashara , ajali za magari mbeya, MV Spice Islander , Mv High Randers na Kivuko cha Ukerewe.

Hata hivyo Abdulkarim Urassa amesema suala hilo lazima litakuwa limegubikwa na wizi kwa wasio waaminifu kwa muda mrefu bila hata Serikali kufahamu, “Sasa si wizi huo, Hazina wenyewe wakati wapo warithi.”

Share.

About Author

Leave A Reply