Saturday, July 20

Wananchi Mirerani waomba kibali cha kuchangia elimu

0


By Joseph Lyimo, Mirerani [email protected]

Mirerani. Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, imeazimia kuomba kibali kwa mkuu wa wilaya hiyo ili wananchi wachangie ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwenye kikao cha baraza la mamlaka hiyo.

Kobelo amesema wamemwagiza mtendaji wa mamlaka hiyo, Evence Mbogo kuandika barua kwa mkuu wa wilaya hiyo Zephania Chaula ili wapatiwe kibali hicho.

Amesema wananchi wanapaswa kupendekeza kiwango cha kulipa ili kumalizia majengo ya wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

“Bado hatujaweka kiwango maalum kati ya Sh5,000 kwa kila mtu au Sh5,000 kwa kaya ila kamati ya fedha na uongozi itakutana ipange hilo na kuanza masomo,” amesema Kobelo.

Amesema shule mpya ya sekondari, Songambele inatakiwa kuendelea kujengwa ili wanafunzi waingie na waendelee na masomo ya kidato cha kwanza.

Ofisa Tarafa ya Moipo, Joseph Mtataiko amesema shule ya sekondari Songambele ya kata ya Mirerani, imeshapata usajili hivyo itaanza na wanafunzi 200 wa kidato cha kwanza.

Mtataiko amesema idara ya elimu ya wilaya hiyo imeshapewa kibali na Tamisemi hivyo wanafunzi hao 200 watapunguza mrundikano kwenye shule ya sekondari Mirerani Benjamin Mkapa.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Tanesco, Justin Abraham amesema wananchi wanapaswa kuchangia fedha na wakishirikishwa hawapingi kwani ni wapenda maendeleo.

“Tutawaelewesha wananchi wetu wataelewa tu na watachanga fedha zao kwa ajili ya manufaa ya watoto wetu ili waweze kupata elimu,” amesema Abraham.

Share.

About Author

Leave A Reply