Friday, July 19

Wakulima korosho waja na ombi jingine kwa Magufuli

0


Tunduru. Baadhi ya wakulima wa korosho wanahisi kutakuwa na ongezeko la bei ya pembejeo mwakani baada ya Serikali kuamua kununua mazao yao kwa Sh3,300 na hivyo wanamuomba Rais John Magufuli asaidie kudhibiti hali hiyo isitokee.

Serikali iliingilia kati ununuzi wa korosho baada ya wakulima kugoma kuuza kwa bei ya chini ya Sh3,000 iliyopendekezwa na wafanyabiashara kutokana na bei ya zao hilo duniani kushuka.

Wakizungumza na Mwananchi juzi jioni baada ya kulipwa fedha zao katika Kijiji cha Mtonya wilayani Tunduru, wakulima hao walidai kuwa wafanyabiashara wa pembejeo watapandisha bei kwa sababu wanajua wakulima watakuwa na fedha kutokana na kuuza korosho kwa bei nzuri.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kwa kununua korosho hizi maana hali ilikuwa mbaya,” alisema mmoja wa wakulima hao, Issa Yassin aliyedai anawakilisha wenzake.

“Lakini sasa tunakwenda kukumbana na changamoto ya bei ya pembejeo kupanda. Rais atusaidie kuwadhibiti kama alivyofanya kwenye bei ya kuuzia.”

Lakini, mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera aliwapa mbinu ya kununua mapema kukabiliana na hali hiyo.

“Hapa ni mwendo wa mafiga matatu. Unapata fedha, unanunua pembejeo na zilizobaki unafanya matumizi mengine,” alisema Homela.

Akizungumzia utaratibu wa malipo, Yassin alisema mchakato umekwenda vizuri na haujachukua muda mrefu baada ya kumaliza kuhakikiwa majina na korosho walizopeleka kuuza.

Mkulima mwingine, Shaibu Said aliungana na Yassin kumshukuru Rais Magufuli, akisema amewapa unafuu wa maisha baada ya Serikali kuamua kununua korosho zao kwa bei nzuri.

Zao la korosho limeongezeka umaarufu katika kipindi kifupi na mwaka jana wakulima waliuza hadi Sh4,000 kwa kilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu (BoT), mauzo ya korosho kwa mwaka ulioishia Machi, 2017 yalifikia dola 340 milioni za Kimarekani, ikiwa ni ongezeko la takriban mara mbili kutoka dola 187 milioni.

Share.

About Author

Leave A Reply