Tuesday, August 20

Wakristo watakiwa kujiweka mbali na uchonganishi

0


By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakristo wametakiwa kujiweka mbali na uchonganishi kwani ni chanzo cha kusababisha wengine wakose haki.

Wito huo umetolewa leo Aprili 19, 2019 na Msaidizi wa Askofu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chidiel Lwiza wakati wa ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kwenye usharika wa Azania Front.

Amesema suala la uchonganishi linaonekana kushika kasi na watu wanaamua kuchukua hatua bila kujiridhisha na wanayoambiwa.

“Kama Yesu alivyosingiziwa maneno ya uchonganishi hilo suala pia linaonekana ndani ya wanadamu, viongozi wanachonganisha na kuchonganishwa, pia raia wanachonganishana.”

“Viongozi wakichonganishwa au kusikiliza uchonganishi watashindwa kusimamia haki kama ilivyokuwa kwa Pilato na hatimaye Yesu akasulubiwa,” amesema.

“Tunapaswa kuwa na moyo wa kusamehe, kama Mungu anatusamehe dhambi zetu sisi ni akina nani tushindwe kusamehe,” amesema.

Mchungaji Chidiel pia amegusia suala la kutunza utu wa watu na kusisitiza kuwa hakuna sababu inayoruhusu binadamu ateswe na kudhalilishwa.

“Utu wa mtu unapaswa kutunzwa, Yesu aliteswa na kudhalilishwa lakini mateso hayo yasiwe sababu ya watu kuteswa kwa sababu ya imani au misimamo yao,” amesema.

“Na wewe unayedhalilishwa au kuzungumziwa vibaya usisahau wajibu wako, Yesu alipigwa na kudhalilishwa lakini alikumbuka kuhusu mama yake na kumuelekeza mwanafunzi wake amtunze, tunapaswa kuwa na imani kuwa siku zote Mungu yuko pamoja nasi,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply