Sunday, August 18

Wakristo watakiwa kuitumia sala kama silaha yao

0


By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Askofu wa Jimbo la Katoliki Kayanga, Almachius Rweyongeza amewakumbusha waumini kuzingatia amani, sala kwa Mungu wakati wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka.

Akifafanua kuhusu sala, askofu Rweyongeza alisema sala inafariji, na kuwataka watu waitumie katika maisha yao kama silaha.

Katika ibada ya Pasaka kitaifa iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu George, Karagwe leo Aprili 21, 2019 askofu huyo pia amesisitiza kuhusu amani.

“Amani ndiyo ujumbe wa Yesu Kristo kwetu sote hivyo tunaposherehekea ni vyema tukatakiana amani ambayo inatokana na msalaba,” amesema.

Amesema Yesu alituachia zawadi ya amani akimnukuu,  “nawaachieni amani, nawapeni amani yangu siwapi ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo.”

Askofu Rweyongeza amesema amani si tu kutokuwepo kwa vita wala si matokeo ya utawala wa mabavu bali inaitwa kwa usahihi kamili kazi ya haki.

 “Kila mtu azitawale tamaa zake na Serikali ijihusishe katika kulinda amani, Pasaka ni wakati wa kufanya tathmini juu ya maisha yako, iwe mtu binafsi, iwe taifa kama wanaendelea kuikumbatia amani ya Kristo ama la.”

Pia amewahimiza waumini kufanya tathmini ya maisha yao kwa sala kwani sala inafariji, inatia moyo na kamwe mtu hatokwama  katika shughuli zake, maisha yake kama atatumia silaha ya sala.

“Tatu, fanyeni tathmini ya maisha ya sakramenti, Tumuombe Mungu aendelee kutusaidia kuadhimisha na kupokea sakramenti tusije tukakosa manufaa yake,” amesema Askofu Rweyongeza.

Amesema “Tukumbuke mapambano ya kiroho ni ya sote, ikumbuke kanuni ya chama cha Tanu isemayo binadamu sote ni sawa Afrika ni moja, Sote tupo kwenye mapambano ya kiroho.”

Kadhalika amewataka waumini kufanya tathmini juu ya vipaji na karama zao kwani vipaji hivyo si kwa ajili yao bali ni kwa ajili ya watu wengine.

“Mti hauli matunda yake, unatoa matunda kwa ajili ya wengine, na wewe hupaswi kujinufaisha binafsi, vipaji na karama ulizopewa na Mungu umepewa bure toa bure, maandiko matakatifu yanasema ni heri kutoa kuliko kupokea.”

Ameongeza kuwa taifa lifanye tathmini juu ya adui ujinga na kupambana naye kwa silaha ya elimu.

“Tunapojitahidi kuleta maendeleo ya pamoja tusisahau kujenga dhamiri kwa watoto wetu, maandiko matakatifu yanasema dhamiri ya mtu ni taa ya Mwenyezi Mungu,” amesema.

Share.

About Author

Leave A Reply