Tuesday, August 20

Wakenya wang'ara Ngorongoro Half Marathon

0


By BERTHA ISMAIL

ARUSHA. Wanariadha kutoka Kenya wameendeleza ubabe wao wa kukata upepo dhidi ya wanariadha wa Tanzania  baada ya kuongoza tena katika mbio za Ngorongoro Half Marathon zilizofanyika leo Jumamosi wilayani Karatu mkoani Arusha.

Mbio hizo zilizofanyika jana kuanzia geti kuu la kuingia Hifadhi ya Ngorongoro hadi Uwanja wa Mazingira bora, ziliongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Karatu kwa lengo la kuhamasisha utalii na kupinga ujangili zilizoandaliwa na Kampuni ya Meta Sports Promotion.

Kwa upande wa wanaume waliokimbia umbali wa kilomita 21, aliyeibuka mshindi ni Mkenya Abraham Too aliyetumia saa 1:05:39, akifuatiwa na Michael Kishimba kutoka Tanzania aliyetumia saa 1:05:45 na nafasi ya tatu imechukuliwa na Mkenya Festus Cheboi aliyetumia saa 1:05:47.

Nafasi ya nne imechukuliwa na Baraka Ramadhani aliyetumia saa 1:06:06 na nafasi ya tano ni Shing’ade Giniki aliyetumia saa 1:06:29 wote kutoka Tanzania.

Kwa upande wa wanawake pia imeongozwa na mwanariadha wa Kenya Esther Chesang’ aliyetumia saa 1:16:41 na nafasi ya pili ni Nathalia Elisante aliyemaliza kwa saa 1:16:49 na nafasi ya tatu ni Anjelina Tsere aliyetumia saa 1:18: 57 wote kutoka Tanzania.

Nafasi ya nne kwa wanawake imeshikwa na Amina Mgoo aliyemaliza kwa saa 1:20: 07 na Monica Cherita aliyetumia saa 1:21:08 Akizungumza mara baada ya ushindi huo Nathalia Elisante alisema kuwa ushindani wa wenzao kutoka Kenya ni mkubwa lakini uwekezaji katika mchezo huu utaweza kuwafanya kuwa zaidi yao.

“Tanzania vipaji vipo sana tu, tatizo ni uwekezaji wa wanariadha wanaoonyesha uwezo na vipaji vya riadha kuendelezwa sambamba na maandalizi katika mashindano mbali mbali ya kitaifa na kimataifa ili kuwaongezea uwezo.”

Share.

About Author

Leave A Reply