Saturday, August 24

Wagosi wakiri kujipunja kwa Alikiba

0


By OLIPA ASSA

MWENYEKITI wa Coastal Union, Steven Mnguto ameshindwa kujizuia na kufunguka namna walivyokuwa na matarajio makubwa ya kiuchumi kupitia mshambuliaji wao, Ali Kiba na kukiri kuwa hawajamfaidi kama ilivyokuwa ndoto zao.

Mnguto amesema walimsajili supastaa huyo anayeimba muziki wa kizazi kipya kwa sababu mbili. Kwanza, kubebwa na ukubwa wa jina lake na kuwaingizia kipato kupitia mechi zao za nyumbani kutokana na utaratibu wa sasa wa wenyeji kubeba mapato yote. “Tulichopata ni kiduchu kuliko tulichokitarajia, ila si kosa la Kiba kwani alituweka wazi ratiba zake za kazi kama unavyojua yeye ni mwimbaji hivyo alikuwa na mambo mengi.

“Mtihani ulikuwa unakuja pindi tunapotaka kucheza mechi za ugenini tulikuwa tunashindwa kumtumia kwani tungekuwa tunawanufaisha wengine labda tungekuwa tunafanya makubaliano na wenyeji wetu ya kugawana mapato.

“Kuna wakati pia kwenye mechi za nyumbani unakuta ndio ametoka safari, mwili wake unakuwa hauna mazoezi ya kutosha kwa kocha mwenye taaluma yake kama Juma Mgunda hawezi kumpanga, kwani anakuwa anasaka matokeo kwa wakati huo, hiyo ndio sababu ya kutofaidika naye tofauti na matarajio yetu,” alisema.

Awali ilisemekana Alikiba aliwekeza Coastal kupitia kinywaji cha Mofaya Energy, lakini Mnguto amekanusha hilo kwamba makubaliano yalikuwa ni kuinua uchumi kupitia mechi za nyumbani na jina lake kuibeba timu.

Alipoulizwa kama msimu ujao watamuongezea mkataba? Mnguto alijibu kuwa, “tunaenda kulijadili kwenye kikao chetu cha uongozi tujue namna ambavyo tutafaidika na huduma yake.”

Naye Kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda alisema ratiba za Ali Kiba zilimbana, lakini akakiri kwamba ni mchezaji mzuri.


Share.

About Author

Leave A Reply