Sunday, August 25

Wafanyabiashara walia bei ya mifuko mbadala

0


By Aurea Simtowe,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wafanyabiashara wadogo wa nyanya, bidhaa za nyumbani na wamachinga wameiomba Serikali kutafuta mifuko mbadala ya bei rahisi itakayowawezesha kuwafungia wateja bidhaa wanazonunua.

Wameyasema hayo leo Mei 27, 2019 wakati wakizungumza na Mcl Digital katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Ombi hilo limekuja zikiwa zimesalia siku nne kabla ya kufikia mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo itakayoanza rasmi Juni 1.

Akizungumza na Mwananchi, Mfanyabiashara wa nyanya Moureen Chau amesema hadi sasa hajajua ni kitu gani atakuwa akitumia kuwafungia wateja bidhaa watakazonunua kutokana na mifuko mbadala kuwa bei ya juu.

“Mimi nanunua nyanya boksi Sh70,000 faida ninayopata haifiki Sh20,000 ninapopanga kwa mafungu na katika hiyohiyo faida ninunue mifuko mbadala ambayo ya bei ndogo ni Sh100 kila mmoja nitapata kitu gani hapo.”

“Zamani tulikuwa tunanunua mifuko ya Sh700 ile milaini inakuwa 50 ndani yake unaitumia huenda hadi biashara unamaliza lakini sasa hii hadi nipate hiyo mifuko 50 lazima niwe na Sh5,000.” Amesema Maureen.

Mmoja wa machinga katika soko hilo, Yasir Ndauka amesema ili kuondokana na gharama za kuwapatia mifuko hiyo wateja watalazimika kutumia mifuko inayokuja na nguo hadi pale bei itakaposhuka.

“Mpaka sasa bei ni Sh100, nauza nguo ngapi kwa siku ili niweze kuwapatia wateja wangu wote mifuko hiyo na faida ninayoipata mimi si kubwa kiasi hicho.” Amesema Ndauka.

Mmoja wa wauzaji wa mifuko ya rejareja maarufu kama Kariakoo, Sikitu Mussa amesema soko la mifuko mbadala bado si kubwa ukilinganisha na mifuko ya Rambo hata faida yake ni ngumu kuiona kwa wakati.

“Sisi tunalazima kuuza kuanzia Sh300 ili tupate faida kwa sababu hii ndiyo angalau mikubwa sasa wengi walikuwa wakinunua mifuko ya Sh200 hivyo bado biashara siyo nzuri labda katazo likianza rasmi.” Amesema Mussa.

Share.

About Author

Leave A Reply