Friday, March 22

Wafanyabiashara wadogo EAC walia na marufuku

0


Wafanyabiashara ndogondogo wanaofanya shughuli zao maeneo ya mipakani katika nchi za Afrika Mashariki, wamelalamikia kuumizwa na uamuzi wa baadhi ya nchi ndani ya jumuiya hiyo.

Hali hiyo imesababisha wengi wao kushindwa kunufaika na kutumia vyema fursa zinazojitokeza ndani ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-CM), ambalo limefungua milango kwa usafirishaji huru wa bidhaa na huduma.

Wakizungumza kwenye mafunzo ya kuwanoa wakufunzi kuhusiana na mwongozo unaowalenga wafanyabiashara wadogo na wakati wanawake katika maeneo ya mipakani, wafanyabiashara hao wanasema mabadiliko ya ushuru wa forodha na marufuku ya mara kwa mara miongoni mwa nchi wanachama ni kikwazo kikubwa kwao.

“Wafanyabiashara wadogo wanawake na makundi ya watu yasiyo na fursa ndiyo wajasiriamali wakubwa, ndiyo wanaotarajiwa kuwa wanufaika wakubwa kama EAC itajitahidi kupanua wigo wa utoaji elimu kuhusu sheria za mipakani,” anasema Dk Kirsten Focken, kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) anayehusika na EAC.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa mipakani kutoka Kenya, Florence Atieno anasema uamuzi unapofanywa na baadhi ya nchi wanachama katika vikao vya juu, taarifa zake haziwafikii kwa wakati mwafaka.

Anasema hilo huwasababishia hasara kwa vile hulazimika kutumia fedha nyingi kukidhi mabadiliko ya mambo kadhaa yahusuyo biashara za pamoja.

Atieno, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha kuweka na kukopa (Sacco) chenye wanachama 600 katika Kaunti ya Busiya, Kenya, anasema Serikali zinapaswa kuwafahamisha mapema wafanyabiashara wa aina hiyo wanaoendesha biashara za mipakani, hata kabla ya uamuzi kufanyika ili kuepusha athiri katika shughuli zao.

Naye Mwenyekiti wa chemba ya biashara ya wanawake kutoka Kilimanjaro (TWCC), Joyce Ndossy alisema wakulima wa mahindi wa Tanzania wanaumia kutokana na uamuzi wa ghafla wa kupiga marufuku usafirishaji wa zao hilo nje ya nchi.

Kwa sasa gunia moja la mahindi nchini linauzwa kati ya Sh18,000 na Sh25,000, lakini kulingana na Ndossy, bei ingekuwa zaidi ya hapo kama Serikali isingepiga marufuku usafirishaji nje.

Anasema licha ya kuwapo kwa sababu za msingi kuhusiana na marufuku hiyo, kutokuwapo kwa taarifa miongoni mwa wafanyabiashara, kumewafanya wengi wao kupata hasara.

Wakizungumza baada ya kuzindua kituo cha huduma cha pamoja mpakani (Ones Stop Border Post – OSBP) katika eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais John Magufuli na Uhuru Kenyatta waliwataka Watanzania na Wakenya kuongeza biashara kupitia mipaka ya nchi hizo hasa Namanga, huku wakiagiza wafanyabiashara wadogo kutobughudhiwa.

Wafanyabiashara hao wanasema viongozi wa juu kama marais, hutoa maagizo kwa wasaidizi wao ili wayashushe kwa walioko chini, lakini hayatekelezwi ipasavyo.

Hivyo, wengi wao wanasema hujikuta wakipata hasara hasa inapotokea nchi kuingia katika mikwaruzano ya kibiashara kama hatua iliyochukuliwa na Tanzania Novemba 2017, kupiga marufuku vifaranga vya kuku 6,400 vyenye thamani ya Sh12.5 milioni kuingia nchini kwa madai kuwa viliingizwa kinyume cha sheria.

“Kenya ni ya 3 kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji Tanzania kwa hiyo Wafanyabiashara wa Kenya wanapopita hapa msiwaone ni maadui, halikadhalika Tanzania ina mifugo mingi hasa ng’ombe kwa hiyo Watanzania wanapopeleka nyama Kenya nao wasikwamishwe,” alisema Rais Magufuli katika uzinduzi wa kituo cha Namanga.

Share.

About Author

Leave A Reply