Sunday, August 18

Wadaiwa kutapeli kwa jina la Mama Magufuli

0


By Hadija Jumanne na Pamela Chilongola. [email protected]

Dar es Salaam. Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam wakikabiliwa na mashtaka manne, likiwamo ya kutapeli kiasi cha Sh 4.4 milioni kwa kutumia jina la Janeth Magufuli ambaye ni mke wa Rais John Magufuli.

Pia washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kutakatisha fedha kiasi cha Sh4.5 milioni.

Washtakiwa hao ni  Saada Uledi, Maftaha Shabani, Heshima Ally na Shamba Baila.

Akisoma hati ya mashtaka leo Alhamisi Aprili 18, wakili wa Serikali Batilda Mushi alidai washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 30/2019.

Alidai shtaka la kwanza ambalo ni kula njama, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2017 na Machi 2019 katika jiji la Dar Es Salaam walichapisha taarifa za uongo kupitia akaunti yao ya mtandao wa kijamiii wa Facebook.

Shtaka la pili, washtakiwa wanadaiwa siku na eneo hilo walichapisha machapisho katika akaunti yao ya mtandao wa kijamii wa Facebook, wakionyesha Janeth Magufuli ambaye ni mke wa Rais  Magufuli ameunda taasisi ya kutoa mikopo kwa watu mbalimbali ikiwa na masharti ya kuweka fedha kabla ya kupewa mkopo kama ni kinga ya mkopo huku wakijua kuwa ni uongo.

Shtaka la tatu, wanadaiwa Machi 2 na 8 mwaka huu jijini Dar es Salaam, wakiwa kama waendeshaji wa akaunti hiyo ya Facebook, walisajili akaunti hiyo kwa jina la Janeth Magufuli kwa nia ya kudanganya na kujipatia Sh4,487,000 kutoka kwa Paul Kunambi kama kinga  ya mkopo wakati wakijua kuwa siyo kweli.

Mushi ameendelea kudai katika shtaka nne ambalo ni utakatishaji wa fedha, washtakiwa kwa pamoja kati ya Machi 2 na 8 mwaka huu katika jiji hilo, walijipatia Sh 4, 487,000 huku wakijua kuwa fedha ni zao la  fedha haramu zilizotokana kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yanayowakabili, Hakimu Kasonde alisema hawatakiwi kusema chochote mahakamani hapo kutokana na kesi inayowakabili kuwa ni uhujumu uchumi.

“Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili isipokuwa Mahakama Kuu pekee au kwa kibali maalumu kutoka kwa DPP, hivyo hamruhusiwi kujibu chochote mahakamani hapa,” alisema Hakimu Kasonde.

Upande wa mashtaka ulieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 2 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Share.

About Author

Leave A Reply