Friday, July 19

Wachezaji Yanga walicheza mechi bila kula mchana

0


By THOBIAS SEBASTIAN

Dar es Salaam. ‘Uwezi kuamini lakini ndiyo ukweli’, wachezaji wa Yanga leo walicheza mechi hiyo bila ya kula chakula cha mchana pamoja na kupambana kwa dakika 90 na kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi JKT Tanzania.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema si kama hawakuwa na pesa au chakula bali kubadilika kwa ratiba ya mchezo huo ghafla kumevuruga.

Zahera alisema aliwapa ratiba wachezaji wake kuwa baada ya kunywa chai asubuhi watakula chakula cha mchana saa 08:30, lakini ghafla anapewa ratiba ya mechi kubadilika.

Kubadilika kwa ratiba ya mechi kutoka saa 12:00 mpaka 10:00 ilifanya wachezaji wangu kukosa muda wa kula na ilitubidi muda wa kula tuwe njiani kuja uwanjani.

“Niwapongeze wachezaji wangu siku nane wamecheza mechi tatu katika kiwango kizuri tena mechi hizo tukiwa tunasafiri viwanja tofauti,” alisema Zahera.

“Wachezaji wangu wamecheza bila kula baada ya viongozi au TFF kwa kubadilishia mechi na muda ambao tulitakiwa kula kama mechi ingekuwa saa 10:00 wachezaji walikuwa wamelala na nisingeweza kuwagongea milango na kuwaamsha.

“Kuhusu kuanza mechi ya leo Ibrahim Ajibu nilimfanyisha mazoezi yake binafsi na tofauti ili kuwa katika kiwango bora na alifanikiwa kufanya hivyo ndio maana nilimtumia katika mechi ya leo,” alisema Zahera.

Mapema leo saa 7 mchana TFF ilitoa taarifa kuwa mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitachezwa saa 10 jioni.

Awali kulikuwa kuna mechi zilizopangwa kuchezwa saa 12 jioni na saa 1 usiku.

Mechi zilizopangwa kuchezwa katika muda huo zimerudishwa saa 10 jioni kufuatia mmiliki wa Uwanja wa Taifa kutoa taarifa za kutowashwa taa za Uwanja ambazo zingehitajika kwa mechi hizo za jioni.

Utekelezaji wa taarifa hiyo ya wamiliki wa Uwanja inaanza kutekelezwa leo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Yanga vs JKT Tanzania mchezo ambao awali ulikuwa uchezwe saa 12 jioni.

Share.

About Author

Leave A Reply