Wednesday, August 21

Wachezaji wakigeni waliotikisa Ligi Kuu Bara

0


By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam. Ligi Kuu inamalizika huku mabingwa wakiwa ni Simba baada ya kutangaza ubingwa wakiwa na pointi 93 katika michezo 37 ambayo wamecheza.

Wakati klabu hiyo ikichukua ubingwa, kuna wachezaji waliotoka nje (wageni) wamekuja katika klabu za nchini na wameonyesha uwezo kiasi cha kuzisaidia timu wanazocheza.

Mwanaspoti limewamulika wachezaji hao kwa namna ambavyo wamezisaidia timu hizo mpaka hivi sasa Ligi ikiwa inamalizika.

Usajili wa mshambuliaji Meddie Kagere (Rwanda) akitokea Gor Mahia, mashabiki wengi wa soka nchini walikuwa wakiwabeza na kuona kama vile Simba ilipigwa.

Lakini kadri siku zilivyokuwa zinaenda ndio ubora wake ukaanza kuzidi kuonekana na kuwaziba midomo mashabiki wote ambao walikuwa wanamuita babu.

Kagere katika Ligi Kuu mpaka hivi sasa tayari ameshaifungia timu hiyo magoli 23, huku magoli hayo yakihusika katika kuipa ubingwa Simba msimu huu.

Pia katika kikosi hiki kuna Clatous Chama (Zambia) kiungo ambaye ameonyesha umaridadi katika kupiga pasi, lakini pia katika kutengeneza nafasi za mabao.

Mshambuliaji Emmanuel Okwi (Uganda) ameonyesha uwezo mkubwa katika kutupia wavuni magoli 15 huku yeye, Kagere na John Bocco(16) wakitengeneza kombinesheni nzuri na kuifungia timu hiyo jumla ya magoli 54.

Mshambuliaji Donald Ngoma majeraha yalikuwa yanamchelewesha na kumfanya akae nje ya uwanja kwa muda mrefu. Lakini hata hivyo Azam walimuamini na kumpa mkataba.

Ngoma alianza kucheza katika mzunguko wa pili ameifungia timu hiyo magoli 11, hiki sio kitu kidogo kwake kwani wachezaji wengine ambao walianza Ligi hawakufikisha idadi hii.

Kasi ya Ngoma katika kutupia wavuni imewasaidia Azam kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu.  

Wakati huo huo, Obrey Chirwa (Zambia) naye aliongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji huku wakiwa na kombinesheni nzuri kati yake na Ngoma.

Upande wa kiungo kuna Stephen Kingue (Cameroon) ameonyesha umahili katika ukabaji, mabeki Yakub Mohammed (Ghana) na Bruce Kangwa (Zimbabwe) nao sio habari ndogo kwani wanakaba hadi kivuli wakati huo huo Kangwa ni fundi katika kupiga mipira ya krosi.

Uwezo wa Yakub katika kukaba uliwafanya mabosi wa Simba kuanza kumnyatia, hali hiyo iliwashtua mabosi wa Azam na kuamua kumpa mkataba mchezaji huyo.

Kikosi hiki licha ya kwamba walikuwa wanalia ukata msimu huu nao hawakuwa nyuma katika kusajili wachezaji wa kigeni.

Mshambuliaji Heritier Makambo (DR Congo) alikuwa na msaada mkubwa katika kikosi cha Yanga msimu huu baada ya kuifungia timu hiyo magoli 17.

Uwezo wa Makambo kupamabana na mabeki ulikuwa nguzo nzuri kwani viungo wa Yanga walikuwa na kazi nyepesi kuhakikisha kwamba mipira inafika kwa wakati kwa Makambo.

Kiungo Papy Tshishimbi (DRCongo) naye alikuwa na mchango wake katika eneo la kiungo kwani ameonyesha uwezo katika kukaba pamoja na kupiga pasi za macho licha ya muda mwingine majeraha yalikuwa yanamrejesha nyuma.

Licha ya kuwa na wachezaji hao katika timu za Simba, Yanga na Azam, klabu zingine nazo kuna wachezaji wa kigeni ambao wameonyesha uwezo wao katika kusaidia timu.

Stand kuna Ahmed Tajudin (Alliance) anayecheza kiungo mkabaji, ameonyesha utulivu mkubwa msimu huu, lakini pia Alliance mshambuliaji Brigimana Blaise (Burundi) naye ni miongoni mwa wachezaji waliisaidia timu hiyo baada ya kwenda katika kipindi cha dirisha dogo la usajili.


Share.

About Author

Leave A Reply