Saturday, August 24

Wabunge wawachambua Spika Ndugai, Masele

0


By Ibrahim Yamola, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Uamuzi wa Spika Job Ndugai kuliomba Bunge kumsamehe Mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele baada ya kukutwa na hatia katika makosa manne, umepokewa kwa hisia tofauti na wabunge.

Hatua hiyo ya Spika Ndugai ilikuja baada ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge iliyomhoji Masele Jumatatu iliyopita na kumkuta na hatia katika makosa hayo, kupendekeza kufungiwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge.

Makosa hayo ni kudhalilisha Bunge, kuchonganisha viongozi, kutohudhuria baadhi ya vikao vya mkutano wa Bunge la Bajeti na kusafiri nje ya nchi bila kibali cha maandishi cha Spika.

Juzi, Spika Ndugai aliliomba Bunge kumsamehe baada ya wawili hao kila mmoja kumtuhumu mwenzake ndani ya Bunge, jambo ambalo wabunge waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Bunge, wamelizungumzia kwa mitazamo tofauti.

Masele alimtuhumu Spika Ndugai kutaka kumng’oa kwenye nafasi yake ya Makamu wa Rais wa Bunge la Afrika (PAP), kwa kuwasiliana na viongozi wa bunge hilo, waliokuwa wakimtuhumu kwa utovu wa nidhamu, bila kumsikiliza huku Spika Ndugai akisema Masele amekuwa mchonganishi, mfitini na anagombanisha mihimili.

Katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alisema kama chama, wanashukuru kuona jambo hilo limemalizika kwa amani huku akikataa kuzungumzia suala la kumhoji Masele kama alivyoagiza Spika.

Alipokuwa akiiagiza kamati ya maadili kumhoji Masele, Spika Ndugai aliagiza pia mbunge huyo kuhojiwa na kamati ya maadili ya wabunge wa CCM juu ya sakata hilo.

“Hatua ya Spika kulimaliza kwa busara sisi kama chama tunaunga mkono, kila mtu ameona kwa mara ya kwanza mtuhumiwa amepewa nafasi na amezungumza kila mtu amemsikia,” alisema Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini.

Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji alisema, “tunamshukuru Spika ametumia busara lakini tunashukuru mtuhumiwa ameweka ushahidi hadharani. Nampongeza Masele ameomba radhi na ameonyesha msimamo na Watanzania wamejua ukweli.”

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema kazi ya Bunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi, hivyo Bunge lisipoonyesha utaratibu huo, “tunapaswa kujirudi kwa pamoja na kujitathmini.”

Alisema, “ili Bunge lionyeshe usafi wote, liweke wazi hansard. Tunapaswa kujadili masilahi ya mama Tanzania si kujadili watu.”

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema Spika Ndugai kama alivyofanya kwa kumsamehe Masele, angeweza kufanya kwa wabunge wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Halima Mdee (Kawe) ambao wamefungiwa kuhudhuria mikutano mitatu kwa Lema na Mdee miwili kuanzia mkutano huu.

“Mimi nina miaka tisa ya ubunge, Spika anapaswa kuwa kiongozi, mlezi, sasa alichokifanya kwa Masele kwa nini hakukifanya kwa Lema au Halima? Lakini maelezo yao yanazidisha mkanganyiko sana,” alisema

Mchungaji Msigwa alisema kitendo cha Masele kutaka kuwekwa hadharani hansard, “kama alivyofanya CAG (Profesa Mussa Assad), inaonyesha kuna tatizo”

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati ya maadili, Emmanuel Mwakasaka alipoulizwa kuhusu taarifa za mahojiano alisema hayo ni mali ya Bunge na wao wanachosoma bungeni ni kwa kifupi na mtu akihitaji kwa kina anaweza kuomba.

Share.

About Author

Leave A Reply