Saturday, August 17

Vituo maalum ukaguzi wa mabasi ya umma mbioni kuanzishwa

0


By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma.  Serikali ya Tanzania kupitia Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani imeandaa utaratibu wa kuwa na vituo maalum vya ukaguzi wa mabasi ya umma katika vituo vikuu vya mabasi kila mkoa ambako mabasi ya abiria hufanyiwa ukaguzi kabla ya kuanza safari na yanapofika mwisho wa safari.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Aprili 23, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rose Tweve.

Katika swali la msingi, Tweve alitaka kujua ni lini Serikali itaandaa utaratibu wa kuwa na vituo maalum vya ukaguzi wa magari ya umma ili kusaidia matumizi mazuri ya muda.

Katika majibu yake Masauni amesema, “Aidha ukaguzi wa pembezoni mwa barabara ambao huhusisha mabasi ya daladala na vyombo vingine vya moto hufanyika katika vituo vya ukaguzi maalum ambavyo vipo katika barabara kuu na katika barabara zingine za miji na majiji.”


Katika swali la nyongeza, Tweve alihoji sababu za askari wa usalama barabarani kukamata magari kiholela, kutolea mfano wanaokamata daladala na kuanza kukagua dereva na kondakta kama wamevaa sare, jambo alilodai kuwa linawapotezea muda abiria.

Katika majibu yake Masauni amesema, “Sheria (ya usalama barabarani sura ya 168) inatoa mamlaka kwa askari kusimamisha gari, kimsingi inatokana na baadhi ya madereva kukiuka sheria za barabarani.”

“Mfano kuendesha gari kwa spidi hivyo lazima wachukue hatua. Madereva watii sheria za usalama barabarani na askari wetu wa usalama barabara kama wapo ambao wanasimamisha magari kiholela bila kuwa na makosa yoyote waache mara moja.”

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi katika swali lake la nyongeza alitaka kujua ni lini Serikali itafunga kamera katika barabara kuu zote nchi nzima ili askari wa usalama barabarani waweze kufanya majukumu mengine.

“Katika barabara kuu ya Dar es Salaam-Morogoro tunaona zimefungwa kamera kwa nini kamera hizi zisifungwe nchi nzima ili askari warudi vituoni wakaendelea kushughulika na kukamata wahalifu,” amesema Sugu.

“Hawa askari wa usalama barabarani wanakaa kwa ajili ya kufuatilia mwendokasi wa magari, sasa kamera hizo zitaweza kubaini mambo hayo na taarifa kukusanywa na madereva watafuatwa walipo kulingana na taarifa za magari yao.”

Akijibu swali hilo la nyongeza Masauni amesema, “Huo ndio mwelekeo wa Serikali yetu na mambo ya kibajeti yakikaa vyema tutafunga kamera nchi nzima. Ni suala la kuvuta subira na jambo hilo litafanyika hatua kwa hatua.”

Share.

About Author

Leave A Reply