Wednesday, August 21

Viongozi wa umma watakiwa kuzingatia maadili

0


By Filbert Rweyemamu,mwananchi [email protected]

Longido. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini imesema viongozi wa umma wasipozingatia viwango vya maadili vilivyoanishwa  kwenye sheria zipo athari zinazoweza kulipata taifa zikiwemo kupungua kwa imani ya wananchi kwa serikali yao pamoja na kuathiri mshikamano na umoja wa kitaifa.

Akizungumza katika mafunzo ya viongozi hao leo, Katibu Msaidizi wa

Sekretarieti hiyo, Anna Mbasha alisema jukumu la viongozi wa umma ni

kuhakikisha wanasimamia na kutekeleza sheria hivyo kikamilifu bila kufanya hivyo  itasababisha kuwepo kwa matumizi ya rasilimali za umma yasiyofaa hivyo kukua kwa kiwango cha umaskini katika jamii.

“Viongozi wa Umma wasipozingatia maadili inasababisha kupungua kwa dhana ya uzalendo, utaifa, nidhamu, uvumilivu na uwajibikaji mambo yanayoathiri ukuaji wa demokrasia ,utawala bora na ustawi wa nchi na watu wake,” amesema Mbasha.

Kuhusu zawadi kwa viongozi wa umma alisema yapo makatazo yanayozuia viongozi wa umma kujinufaisha kiuchumi kwa kupokea zawadi kutoka kwenye makampuni yanayofanya biashara na serikali na kwamba iwapo mtumishi atapewa zawadi inayozidi thamani ya sh 200,000 ni muhimu  kutoa taarifa kwa mkuu wake.

Alisema lengo la sheria hiyo haikatazi ukarimu kwa watumishi na

viongozi bali inalenga kuziratibu zawadi hizo ili zisiwe na lengo la

kutoa upendeleo kwa anayezitoa na kusababisha manung’uniko kwa umma.

“Ili kuwa na viongozi waadilifu ni muhimu suala la maadili liwe ni

suala mtambuka, Sekretarieti ya Maadili itaendelea kushirikiana na

wadau mbalimbali katika kujenga na kuimarisha maadili katika ngazi ya

familia hadi ngazi ya taifa,” amesema Mbasha.

Katibu Tawala wa wilaya ya Longido, Toba Nguvila alikemea mgongano wa maslahi kwa watumishi wa umma na wanasiasa hasa katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuwapa uelewa watumishi na madiwani namna ya kuepuka kujiingiza kwenye migongano ya kimaslahi kwa lengo la kutekeleza sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inatoa haki kwa kila kiongozi.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Jumaa Mhina alisema

kumekua na hofu kwa viongozi wa umma wanapoitwa kwenye sekratarieti ya maadili ya umma jambo ambalo hawapaswi kuwa na hofu kwasababu ofisi hiyo ipo kwahudumia watu wote kwa kuzingatia maadili na sheria za nchi.

Share.

About Author

Leave A Reply