Sunday, August 18

VIDEO: Mashuhuda waeleza wachimbaji moramu walivyofukiwa na kifusi

0


By Filbert Rweyemamu na Husna Issa, Mwananchi [email protected]

Arusha. Simanzi  na vilio vilitawala baada ya wachimbaji watatu wa Moramu kuangukiwa na kifusi katika machimbo yaliyopo kata ya Moshono jijini Arusha na aina ya Fuso kuharibika kabisa kwa kufukiwa na kifusi hicho. 

Tukio kama hilo lililotokea jana lilitokea mwaka 2013 na kupoteza maisha ya wachimbaji tisa huku wengine wakijeruhiwa na waziri mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda alishauri utafutwe utaratibu utakaowezesha uchimbaji salama. 

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Joramu Laizer jana alisema baada ya tukio hilo kulitokea sintofahamu hali ambayo ingesababisha madhara makubwa zaidi kama kikosi cha zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na polisi wasingewatuliza mamia ya wananchi. 

“Hapa kulifurika watu baada ya taarifa kusambaa kuwa kuna watu wengi wamefukiwa, kila mmoja alifika kuona kama kuna anayemfahamu aliyenaswa tukaambiwa ni watu watatu ndio wanaoopolewa, tunaomba Serikali iweke miundombinu rafiki ili yasiendelee kupoteza maisha ya watu, ” amesema Laizer. 


 Shuhuda mwingine, Awadhi Kambi amesema alifika katika eneo la tukio na kuwaona majeruhi wawili wakiopolewa na askari wa kikosi cha zimamoto na uokoaji na kukimbizwa katika Hospitali ya Mount Meru . 

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amesema eneo la machimbo hayo  linafaa kuwekewa utaratibu utakaowezesha kuwapo usalama wakati wote kutokana na umuhimu wake wa kupata moramu kwa ajili ya shughuli za ujenzi na idadi kubwa ya ajira iliyopo eneo hilo. 

“Mwaka 2013 walipoteza maisha vijana 13  na waziri mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda alipendekeza njia za kuboresha usalama bila kufunga mgodi huu, tutashauriana na viongozi wenzangu tuone njia sahihi lakini sipendekezi kufungwa ,” amesema.

Wakati wa shughuli za uopoaji kampuni ya ujenzi ya Beijing Construction Engineering Group Co Limited ilitoa mitambo yake mitatu kusaidia shughuli za uokoaji na kusimamisha kazi ya uboreshaji wa mtandao wa maji jijini hapa kwa muda. 

Meneja mradi huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (Auwsa), Guo Xiangke amesema baada ya tukio hilo waliona ni muhimu kushirikiana na Serikali kuwaokoa walionaswa na kifusi hicho. 

Mkuu wa  wilaya Arusha, Fabian Daqarro amesema tukio hilo limewasikitisha na watakaa kikao kwa ajili ya kutoka na uamuzi wa namna ya kuwezesha wananchi kufanya kazi kwa njia za usalama zaidi na taarifa zaidi zitatolewa. 

“Tunashukuru kazi ya kuiondoa miili imefanikiwa na majeruhi wamepelekwa Hospitali ya Mount Meru ni jambo la huzuni, tutawajulisha hatua tutakazochukua baadaye, ” amesema Daqarro.

Share.

About Author

Leave A Reply