Monday, August 26

VIDEO: Kelvin John: Hatma yangu kucheza soka kulipwa ni Juni

0


By Saddam Sadick

Mwanza. Nyota wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Kelvin John amesema hatma yake ya kujua ni timu gani ataichezea msimu ujao itajulikana mwezi ujao.

Mshambuliaji huyo amekuwa na kiwango bora katika kikosi cha Serengeti Boys jambo lililomfanya ajumuishwe katika kikosi cha awali cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kitakachoshiriki Afcon mwezi ujao nchini Misri.

Akizungumza katika mahojiano maalumu chipukizi Kelvin alisema hawezi kutaja wazi timu atakayoichezea hadi Juni mambo yatakapokuwa yamekamilika.

Alisema yeye ana Meneja wake anayesimamia mchakato mzima wa kujua ni timu gani atachezea na kuweka wazi kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri.

“Mimi umri wangu bado mdogo sijafikia kuzungumza na timu yoyote kusaini kucheza, ndio maana nasema nina Meneja wangu anayesimamia kila kitu na mazungumzo yanakwenda vizuri kwa timu zinazonihitaji hivyo kufikia mwezi wa sita nitajua,” alisema mshambuliaji huyo.


Pia alifafanua kuwa kuitwa kwake kikosi cha Stars anaamini atamshawishi Kocha Emmanuel Amunike na kwamba hiyo ni fursa kwake kuonyesha uwezo ili kupata nafasi.

Straika huyo hakusita kueleza timu anazovutiwa nazo ikiwa ni Kaizer Chief ya Afrika Kusini pamoja na Real Madrid ya nchini Hispania na kwamba siku ikifika ndoto zake zitatimia.

“Hatukufanya vizuri Afcon ya vijana kwa sababu tulizidiwa uwezo, lakini naamini kocha aliona mapungufu zaidi,” alisema Kinda huyo.


Share.

About Author

Leave A Reply