Friday, August 23

VIDEO: ‘Changamoto za Muungano hazitakwisha’

0


By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar leo ukitimiza miaka 55, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema si rahisi kumaliza changamoto zote.

Kauli ya Waziri Makamba imekuja wakati kukiwa na orodha ya kamati zilizowahi kuundwa kushughulikia kero za Muungano bila kufanikiwa kuzimaliza.

Miongoni mwa kamati hizo ni pamoja na ile ya Baraza la Mapinduzi (ya Amina), ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (ya Shamhuna, 1997) na ya Rais iliyochambua Ripoti ya Jaji Robert Kisanga (Kamati ya Salim Juma).

Nyingine ni Kamati ya Rais ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) juu ya Kero za Muungano, Kamati ya Ramia (2000) na ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 – 1999).


Akizungumza juzi katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Dar es Salaam, Waziri Makamba alisema tangu awali Muungano ulikumbwa na changamoto na baadhi zimeendelea kuwapo. “Hakutakuja kuwa na mwisho wa kero za Muungano hata siku moja na kama umuhimu au uhalali wa Muungano unaufungamanisha na wingi au uchache wa changamoto, basi huelewi uhusiano wa watu,” alisema Makamba.

“Kwa hiyo mtu yeyote atakayekuhakikishia kuwa huko mbele hakutakuwa na changamoto atakuwa anakudanganya.”

Huku akitoa mfano wa Marekani, alisema kutoisha kwa kero hakumaanishi kwamba Muungano ni dhaifu, bali ndiyo hali yenyewe.

“Marekani wana muungano wa miaka zaidi ya 200 mpaka leo ukisikia moja ya aspirations (mahitaji) za Marekani ni ‘to get to the perfect union’ (kuwa na muungano sahihi),” alisema waziri huyo alipokuwa akizungumzia Muungano ulioasisiwa Aprili 26, 1964.

“Kwa hiyo hata sisi miaka 55 bado kazi ni kuendelea kuutafuta Muungano bora.”

Alipoulizwa kuhusu matokeo ya tume mbalimbali zilizoundwa kushughulikia changamoto hizo ikiwemo ya Jaji Francis Nyalali iliyotafuta maoni ya mfumo wa vyama vingi, ya Jaji Robert Kisanga na ya Jaji Joseph Warioba zilizokosoa Muungano wa Serikali mbili, alisema busara za waasisi zilikuwa bora zaidi.

“Mimi naamini kwamba busara ya waasisi inashinda busara ya Kisanga na Nyalali. Ndiyo jibu langu fupi. Kwa sababu wao walitafakari yote hayo, hawakuwa wajinga,”alisema.

“Hao watu (waasisi) walikuwa genius (wana akili sana), walikuja na fomula ambayo haikuwepo popote duniani na Muungano umeendelea kuwepo kwa miaka 55…nakwambia waasisi walikuwa sahihi.”

Kuhusu suala la Zanzibar kuruhusiwa kukopa lililozua mjadala bungeni hivi karibuni, Makamba alisema kuna kamati ya wataalamu imeundwa kuangalia mlingano wa kisheria na kikatiba ili iruhusiwe kukopa bila kupata ruhusa ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema hoja hiyo haikuanzia bungeni, bali ilitolewa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kuwa ilitaka iruhusiwe kukopa.

“Kwa sababu moja, Zanzibar ina mpango wa maendeleo, kabla ya hapo kulikuwa na Mkuza (Mpango wa Kukuza Uchumi Zanzibar) na ile mipango inahitaji rasilimali.”

Alisema licha ya Zanzibar kuruhusiwa kukopa kila ilipoomba, lakini tatizo ni kucheleweshwa na kutokuwa na uhakika wa kupata ili kutekeleza miradi yake.

“Lilipokuja mara ya kwanza, ilionekana kuna hoja na kwamba ni rasilimali za maendeleo na kitu muhimu ni uhakika wa kupata mkopo. Kama unatafuta fedha na anakukopea mwingine, huna uhakika kama utapata au utakosa.

“Kwanza haijawahi kutokea Zanzibar inataka kukopa halafu dhamana ikakataliwa hata siku moja, lakini kilichokuwa kinazungumziwa ni uharaka na urahisi wa utaratibu wa Zanzibar kukopa kwa dhamana ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Alisema kutokana na hoja hiyo, iliwekwa mikakati ya kurahisisha ukopaji huo ikiwa pamoja na kuunda timu ya wataalamu.

“Imetumwa timu ya wataalamu kuangalia mlinganyo kati ya matakwa ya Katiba na sheria na haja na hoja ya msingi ya Zanzibar kuwa na msingi wa kuwa na rasilimali zake. Sasa ile technical team haijafika mwishoni,” alisema.

Alitoa mfano wa suala la uchimbaji wa gesi kuwa ni miongoni mwa mambo ya Muungano na kwamba lilishapewa ufumbuzi bila kuathiri matakwa ya Katiba.

Kuhusu malalamiko ya kulipa kodi mara mbili kwa watu wanaonunua bidhaa Zanzibar na kuzileta Bara, Makamba alisema awali kulikuwa na ukadiriaji tofauti kati ya vituo vya kodi vya Bara na Zanzibar, japokuwa suala hilo ni la Muungano.

“Kwa hiyo ilikuwa ukiingiza bidhaa kutoka Zanzibar, unapata kwa bei ya chini. Watu walikuwa wakisema wanakwenda kufungasha. Wakifika Bara walikuwa wanakadiriwa ile tofauti. Ile tofauti ndiyo inaitwa kodi mara mbili. Sasa hilo tatizo tumelimaliza kwa sababu tumeweka mfumo sawa,” alisema.

Share.

About Author

Leave A Reply