Monday, August 26

UVCCM kuwapambania walimu wanaojitolea kupata ajira, posho

0


By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM),  Galila Wabanhu amesema zikitoka nafasi za ajira ya walimu watakaopewa kipaumbele ni wale wanaojitolea kufundisha.

Wabanhu ametoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 21, 2019 baada ya kusikiliza changamoto wanazokutana nazo walimu hao wawapo kazini.

Amesema shule nyingi zina upungufu wa walimu, ingawa Serikali inapambana kutatua changamoto hiyo, lakini uhitaji bado ni mkubwa.

Ameeleza kuwa wao kama UVCM wana nafasi ya kufanya ushawishi kwa Serikali zinapotoka nafasi za ajira za walimu, kipaumbele kiwe walimu hao wanaojitolea.

“Lakini kwanza kabla ya kufanya jambo lolote, tuwatambue wapo wangapi nchi nzima, ili iwe rahisi hata kupigania maslahi yao.

“Baada ya hapo hatua inayofuata ni kupigania maslahi yao na kwa kuhakikisha angalau basi wanapewa posho za kujikimu,” amesema Naibu Katibu mkuu huyo.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo mwalimu anayejitolea kwenye shule ya Sekondari Makulumla iliyopo Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam , Ngonyani Mathayo amesema baada ya kumaliza mafunzo kwa vitendo ameendelea kufundisha kwenye shule hiyo.

Anasema anafundisha na shule humpatia Sh50, 000 kwa ajili ya kujikimu nauli na fedha ya kula.

“Hii fedha ni ndogo, lakini niliomba ajira mwaka jana na zilipotangazwa nilikosa, kwa sababu hakuna ajira ninaendelea kujitolea licha ya kuwa na shahada ya ualimu,” amesema Ngonyani.

Ngonyani ameiomba Serikali kuwafikiria wanapokwenda kujitolea ili watimize majukumu yao.

Kwa upande wa mwanzilishi na Mratibu wa walimu wanaojitolea, Emijidius Cornel amesema zinapotokea ajira za walimu, wanaojitolea wakumbukwe.

Cornel amesema wameamua kuisaidia Serikali kuendeleza sekta ya elimu nchini kwa kujitolea kufundisha masomo ya sayansi na hesabu shule mbalimbali kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuyapenda, kuyasoma na kuyapa kipaumbele.

Naye mkuu wa shule ya sekondari Makulumla,  Naomy Alimosa ambako  baadhi ya walimu wanajitolea kufundisha amesema wanamsaidia kukabiliana na changamoto ya walimu.

Amesema kwa wanafunzi  1,578 alionao shuleni kwake alitakiwa awe na walimu wasiopungua 80, lakini kwa sasa anao 41 pekee.

Amesema miongoni mwa hao, wapo waliopo kwenye likizo ya uzazi na masomoni, hivyo kubaki na wachache.

“Walimu wa kujitolea wananisaidia sana, changamoto iliyopo ni kuwezeshwa, napenda vijana kwa sababu wanajitolea na muda mwingi wanakaa na watoto.

“Shule yangu haifanyi vizuri hasa masomo ya hesabu, kwenye somo la  baiolojia, nina mwalimu mmoja anafundisha kidato cha pili chenye watoto 500, pia anafundisha  kidato cha nne chenye wanafunzi zaidi ya 40,” amesema .

Amefafanua kuwa kauli ya Tanzania ya viwanda haiwezi kutimia kama hakutakuwa na  wanafunzi watakaopata maarifa shuleni.

Anaiomba Serikali kuliona hilo kama suala la msingi na kuwawezesha vijana wanaojitolea shuleni.

“Kwa sababu wameamua kujitolea tusiwaache hivihivi kwa sababu wanatoka mbali na shule zina uhaba wa walimu, wakipewa posho watajikimu, lakini watatusaidia kupunguza kero ya uhaba wa walimu,” amesema Alimosa.

Share.

About Author

Leave A Reply