Tuesday, August 20

Ushirika nyenzo muhimu kuelekea uchumi wa kati

0


By STAPHORD KWANAMA

Kaulimbiu ya Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Pamoja na mikakati mingine, mfumo wa ushirika unapaswa kuwa wa kipaumbele kutokana na kwamba zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanaoishi vijijini na kipato cha chini.

Kwa mujibu kitabu cha Kiyosaki (2014), watu wa kipato cha chini wanaweza kutengenezwa kuwa matajiri kupitia mfumo wa makundi mbalimbali ya kiuchumi kama vile ushirika kwa hatua ya awali.

Wanachama hupata maarifa, uzoefu na weledi wa kuboresha uchumi wao ndani ya kikundi na baadaye kutumia uzoefu huo kujitegemea kuboresha uchumi binafsi huku wakiwa wanachangia kwa uwazi na moja kwa moja katika uchumi wa Taifa.

Katika kuungana na dhana ya Kiyosaki, mwandishi anaona mfumo madhubuti wa vikundi unaoweza kuwakwamua kwa haraka Watanzania kutoka uchumi wa chini na kufikia uchumi wa kati ni ushirika kutokana na urasmi wake kupitia Sheria nambari 6 ya Vyama vya Ushirika, 2013 na kanuni zake za mwaka 2015, pamoja na uwapo wa mamlaka kamili inayosimamia vyama vya ushirika.

Kwa pamoja tunahitaji kujenga ushirika imara, wenye nguvu na endelevu kwa kuwa na mikakati madhubuti ya kufufua Vyama vya Ushirika vilivyokufa na vinavyosinzia (makala zinanofuata zitatoa mchango wa ushauri na aina ya mikakati inayotekeleza).

Pia, tunahitaji kuendelea kuanzisha vyama vingi vipya vya ushirika zaidi 10,990 vilivyopo sasa.

Mathalani leo hii tuna vijana wengi wamepata mafunzo ya mgambo na JKT, sasa kwa nini wasipewe elimu stahiki ya ushirika, biashara, uongozi, masoko na menejimenti ili waanzishe ushirika wa huduma za ulinzi.

Hali kadhalika, tuna vijana wengi wanamaliza vyuo mbalimbali ikiwamo vyuo vya ufundi kama Veta, wanaweza kupewa elimu tajwa hapo juu na kuanzisha ushirika kutokana na taalum walizopata.

Pia, kuna vijana wengi mtaani na vijiweni hawana kazi wanaweza kupewa elimu, ushauri na mwongozo ili waanzishe vyama vya ushirika vinavyoendana na nguvu kazi yao mathalani utoaji wa huduma za usafi majumbani na ofisini, huduma za chakula, huduma za usafiri na usafirishaji, ufugaji, kilimo, huduma za ushauri wa kitalaam, huduma za masoko na mauzo.

Ni imani yangu watu wanapokuwa katika makundi rasmi ya kiuchumi ni rahisi kwa wadau mbalimbali kama vile wataalam washauri, watafiti, taasisi za fedha, wauzaji malighafi, wanunuzi na walaji kutoa huduma zinazoweza kuchagiza maendeleo ya vyama husika vya ushirika.

Pia, ni rahisi kwa Serikali kutekeleza malengo yake na usimaimizi wa sheria mbalimbali zikiwamo za uwezeshaji wananchi kiuchumi, maendeleo ya biashara, maendeleo ya vijana, walemavu na kina mama, uwekezaji na uuzaji bidhaa nje ya nchi japo kutaja chache.

Hili linawezekana bila kujali changamoto za historia ya ushirika Tanzania ambayo kwa namna moja ama nyingine imepoteza imani ya watu wengi dhidi ya mfumo wa ushirika.

Changamoto hiyo imepunguza ufanisi na mchango wa ushirika katika uchumi mkubwa wa Taifa.

Tunaweza kuboresha ushirika wetu endapo wizara husika na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania itaunda timu ya watalaamu na wabobezi katika ushirika.

Pia, tukiwa na mijadala mbalimbali ya kujadili nini kifanyike kuongeza kasi ya ukuaji na tija ya ushirika nchini tutafanikiwa katika eneo ya vyama vya ushirika.

Mathalani tunaweza kutumia mfumo wa Wizara ya Fedha na Mipango wa mwaka huu kufanya mijadala na wadau kuhusu uboreshaji mifumo ya kodi nchini.

Licha ya vyama vya ushirika kuwa na maendeleo, wanaushirika wanapaswa kutambua umuhimu wake katika maendeleo yao ya kiuchumi na Taifa kwa jumla.

Miaka iliyopita sekta hiyo ilikuwa na maendele makubwa kwa Watanzania hivyo ni muhimu kuendeleza yale yaliyofanywa zamani ili kuimarisha vyama hivi vyenye msaada kwa wananchi hasa katika kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi.

Uchambuzi huu umeandikwa na mchangiaji wa gazeti hili anayepatikana kwa namba ya simu 0753-125474 au barua pepe; [email protected]

Share.

About Author

Leave A Reply