Saturday, August 24

Ushahidi kesi ya ubakaji ulivyosisimua mahakamani

0


By Tausi Ally, Mwananchi [email protected] mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Msichana wa miaka 22 ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi mshtakiwa Joseph Idrisa (47) alivyombaka.

Hayo yamejiri leo Jumatatu Mei 20, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Frola Mujaya na wakili wa Serikali, Aziza Muhina wakati msichana huyo alipokuwa akihojiwa maswali na mshtakiwa Idrisa dhidi ya ushahidi alioutoa katika kesi ya jinai namba 170 ya 2019.

Msichana huyo aliieleza Mahakama kuwa anamfahamu mshtakiwa huyo kwa kuwa Januari 30, 2019 alikwenda nyumbani kwao kwa lengo la kumsaidia kupata kazi ya jeshi.

Amedai kuwa yeye ana taaluma ya uuguzi, hivyo alitaka kuingia jeshini kwa kupitia fani ya michezo lakini akishafanikiwa aendelee na lengo lake la kufanya kazi ya uuguzi.

Msichana huyo ambaye ni shahidi wa upande wa mashtaka, alidai kuwa tukio la yeye kubakwa na mshtakiwa huyo lilitokea Januari 31, 2019.

Alidai mahakamani hapo kuwa anaishi eneo la kati ya kwa Diwani na kwa Mkolemba na kwamba, mshtakiwa huyo siku ya tukio alimpeleka nyumbani kwake kwa lengo la kwenda kujaza fomu.

Akielezea mazingira ya nyumba alikopelekwa, msichana huyo alidai ina vyumba viwili vinavyotazamana na siku hiyo ya tukio, hakukuwa na mtu zaidi yao.

Baada ya shahidi huyo wa upande wa mashtaka kueleza hayo, mshtakiwa Idrisa alimuuliza ni kwa nini siku ya tukio alipofanyiwa kitendo cha kuingiliwa bila ridhaa yake hakupiga kelele.

Akijibu swali hilo, msichana huyo alidai kuwa alipiga kelele lakini hakukuwa na mtu, hivyo alilazimika kwenda kutoa taarifa nyumbani kwa wazazi wake.

Mshtakiwa Idrisa aliuliza swali lingine ni kwa nini alipelekwa hospitali kupimwa yeye peke yake wasipelekwe wote.

Msichana huyo alijibu kuwa hajui.

“Nilikuhonga wali nyama choma na bia na ulisema ukitoka depo  mimi nitakuwa nani wako,” alimuhoji msichana huyo mshtakiwa Idrisa.

Msichana alijibu kuwa yeye halijui hilo.

Mshtakiwa huyo  aliendelea kumuuliza msichana huyo kuwa yeye ana wake wawili anajua hilo.

Mshtakiwa: Mimi na wewe siku hiyo tulikutana na tukaenda Tandika na nikakununulia suruali na nguo ya ndani (chupi) kwa nini ulivipokea.

Msichana: Nilipokea vitu hivyo kwa sababu uliniambia ni vitu vinavyohitajika kwenye mazoezi.

Mshtakiwa: Kwa nini nilikununulia sabuni, mafuta, viazi na nyanya chungu kwa sababu nilijua wewe ni Msambaa na ukavipokea?

Msichana: Si kweli hivyo vitu ulinunua kwa sababu ulisema unapika nyumbani kwako kwa kuwa ulikuwa na njaa.

Mshtakiwa: Kwanini nguo nilizokununulia ulienda kujaribisha nyumbani kwangu wakati ulikuwa unajua mimi na wewe ni jinsia tofauti na unakumbuka njiani ulisema una jina la namba D na una kilo 45.

Msichana: Hilo jina la namba D silikumbuki lakini kilo zangu nazikumbuka kwa sababu nilikuwa nafanya kazi ya u – nesi.

Mshtakiwa: Unajua kuwa tulinunuliana vitu kwa sababu tulikuwa na makubaliano ya kuwa wapenzi na baba yako alikuja kwangu kudai fedha, hivyo huku si kubaka.

Kama nilikubaka, mbona hukupiga kelele, uliingia kwangu kimya na ukatoka kimya  na nikakusindikiza.

Msichana: Hukunisindikiza ila mimi nilitoka mbio kwa sababu hatukukubaliana ndiyo maana  tupo mahakamani hapa.

Hakimu Mujaya aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 24, mwaka huu,  mashahidi wa upande wa mashtaka watakapoendelea kutoa ushahidi wao.

Share.

About Author

Leave A Reply