Monday, August 19

Usajili wa TCCIA Investment wachangia kukuza mtaji DSE

0


Dar es Salaam. Kuorodheshwa kwa Kampuni ya Uwekezaji ya Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA Investment), kumechangia kuongeza ukubwa wa mtaji wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

Katika wiki iliyoishia Machi 16, mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa sokoni hapo ulipanda kwa Sh483 bilioni kutoka Sh22.7 trilioni wiki iliyoishia Machi 9 hadi Sh23.2 trilioni. Pia, mtaji wa kampuni za ndani ulipanda kutoka Sh10.2 trilioni hadi Sh10.3 trilioni.

TCCIA Investment imechangia kukua kwa mtaji huo baada ya kuorodheshwa sokoni hapo Ijumaa iliyopita, ikiwa na mtaji wa Sh30 bilioni ambao umefika Sh32 bilioni.

Kampuni hiyo inakuwa ya 27 kuorodheshwa DSE baada ya kuuza hisa milioni 112.5 kwa Sh400 kila moja. Akizindua uorodheshaji wa kampuni hiyo, naibu katibu mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Amina Shaaban aliipongeza TCCIA kwa kusimamia michango ya wanachama wake walioianzisha mwaka 1999. “Mmekuza mtaji wenu kutoka Sh1.97 bilioni mpaka Sh30 bilioni mwaka jana. Mmefika hapo bila kukopa wala kupata msaada kutoka taasisi yoyote,” alisema Amina.

Ofisa mtendaji mkuu wa TCCIA Investment, Donald Kamori alisema wanachama wa TCCIA walihamasishwa wakakusanya nguvu na kuanzisha kampuni hiyo. “Wengi wetu ni wakulima na wenye viwanda vidogo. Tuliweka nguvu pamoja na leo tunataka Watanzania wengi zaidi washiriki nasi kukuza biashara nchini,” alisema Kamori.

Licha ya TCCIA Investment, kampuni nyingine zilizochangia kukua kwa mtaji wa DSE ni kupanda kwa bei za hisa za Benki ya KCB kwa asilimia 19, Uchumi Supermarket kwa asilima 11 na TCC kwa asilimia saba. Katika wiki iliyoishia Machi 16, kampuni ya TCC iliongoza kwa mauzo ikichangia asilimia 86 ya hisa milioni tatu zilizouzwa na kuingiza zaidi ya Sh5 bilioni. Vodacom ilifuata na Benki ya CRDB.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.