Sunday, August 18

Usajili huu wa simu uwaamshe Nida

0


Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetangaza kuanzia Mei mosi watumiaji wote wa simu za mkononi nchini wanapaswa kusajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya Taifa mfumo utakaouhusisha uchukuaji alama za vidole.

Awali, watumiaji wa simu za mkononi walisajiliwa kwa kutumia vitambulisho vya aina tatu ikiwamo leseni ya udereva, kadi ya mpigakura, kitambulisho cha Taifa au barua ya mtendaji wa kata au kijiji.

Hata hivyo, vitambulisho aina ya leseni ya udereva, kadi ya mpigakura na barua ya mtendaji vimeondolewa wakati mchakato wa upatikanaji wa kitambulisho cha Taifa ukiwa na changamoto nyingi.

Tunasema hivyo kwa sababu baadhi ya wananchi wamelalamikia kasi ndogo ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Jana gazeti hili lilimnukuu mwananchi mmoja aliyesema alijiandikisha tangu mwaka 2015, lakini hadi sasa hajapata kitambulisho.

Rai yetu ni kuwa tangazo la TCRA liwe kengele ya kuwaamsha Nida kwa kuwa hitaji la vitambulisho vya Taifa limeongezeka. Na hitaji la sasa linaonekana ni la haraka zaidi kwa kuwa Watanzania wengi maisha yao ya kila siku yanategemea simu za mkononi.

Japokuwa TCRA hawajaweka wazi ni lini itakuwa mwisho wa usajili kwa kutumia vitambulisho vya Taifa, tunachohimiza ni kuwa Nida inapaswa kuongeza kasi ya utoaji wa vitambulisho hivyo.

Matumizi ya simu za mkononi ni makubwa na yanasaidia katika kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, kuongeza mshikamano kwenye jamii na pato la Taifa. Pia, simu za mkononi zinatumika kama kifaa cha kupata elimu katika masuala ya kilimo, biashara, ufugaji na kupashana habari mbalimbali zikiwamo za maendeleo.

Mbali na kufanya miamala ya fedha, simu za mkononi zimekuwa mkombozi na suluhisho la haraka kwa wanaopata dharura katika maeneo ya mbali au nyakati za usiku.

Tunafahamu simu hizi zimeendelea kuwa msaada kwa wagonjwa wa muda mrefu wanaougulia nyumbani kwa ajili ya kufuatiliwa na madaktari wao ili kuwapa ushauri kutokana na dharura za kiafya zinazowatokea.

Sababu zilizotolewa na TCRA kwamba usajili unalenga kudhibiti wizi na usalama wa wateja, zinapaswa kuungwa mkono kwa kuwa matukio hayo yamekuwa yakiongezeka kila kukicha.

Hakuna anayebisha kwamba miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la matukio ya watu kutapeliwa fedha kwa kutumia simu na ongezeko la matukio ya uhalifu wa utekaji, ujambazi na mauaji.

Tunafahamu matumizi ya simu za mkononi ni maendeleo, lakini ili yakamilike ni muhimu yakaenda sambamba na usalama wa raia na mali zao.

Hivyo, uamuzi wa TCRA umelenga kuwahakikishia wananchi usalama wao na mali zao kwa kuwaepusha na vitendo vya utapeli na uhalifu unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi.

Kwa mantiki hiyo, TCRA imeongeza matumizi ya kitambulisho cha Taifa na umuhimu wake kwa Watanzania.

Kutokana na hali hiyo umuhimu wa kitambulisho hicho umekuwa mmkubwa kwa kuwa maisha ya wananchi ya kila siku yanategemea simu za mkononi, hivyo tunaisihi Nida kuongeza kasi zaidi katika utoaji wa vitambulisho hivyo.

Share.

About Author

Leave A Reply