Saturday, August 17

Upelelezi kigogo wa Tansort haujakamilika

0


By Hadija Jumanne,Mwananchi [email protected]

Dar Es Salaam. Mshtakiwa, Archard Kalugendo ambaye ni Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania  (Tansort) na Mthamini wa Madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu, wanaendelea kusota rumande kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Washtakiwa hao wanaendelea kusota rumande kwa muda wa mwaka mmoja na miezi saba sasa, kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika katika kesi ya uhujumu uchumi namba 54/2017.

Kalugendo na Rweyemamu, ambao ni watumishi kutoka Wizara ya Madini, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Septemba 15, 2017 kujibu shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh2.4 bilioni.

Hata hivyo, leo, Aprili 23, 2019, wakili wa Serikali, Wankyo Simon amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa upelelezi wa shauri hilo upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Simon ameeleza hayo, wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa. “Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka tupo katika hatua za mwisho kukamilisha upelelezi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama upelelezi umekamilika,” alidai Simon.

Simon baada ya kueleza hayo, mshtakiwa Kalugendo aliomba mahakama iwahimize upande wa mashtaka wakamilishe upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.

“Machi 25, mwaka huu upande wa mashtaka walituambia upelelezi umekamilika, leo wanatuambia upelelezi upo katika hatua za mwisho, sisi tunataka wakamilishe kwa wakati ili kesi iweze kuendelea maana tunaendelea kuteseka,” alidai mshtakiwa Kalugendo.

Hakimu Shaidi, baada ya kusikiliza maelezo ya mshtakiwa aliutaka upande wa mashtaka kuhakikisha kuwa wanakamilisha upelelezi kama walivyoahidi. Kesi hiyo imeahirishwa hadi, Mei 7, 2019 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kwa kuwa kesi inayowakabili haina dhamana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

Kwa pamoja na kwa vitendo vyao viovu wakiwa wathaminishaji wa almasi wa Serikali na waajiriwa wa wizara inayohusika na madini waliisababishia Serikali hasara ya Dola 1,118,291.43 ambazo ni sawa na Sh2.4 bilioni.

Share.

About Author

Leave A Reply