Monday, August 19

Unavyoweza kujinasua katikati ya nguvu za giza

0


By Askofu Elias Chesa

Bwana Yesu asifiwe, Jina langu naitwa Askofu Elias Chesa kutoka Kanisa la Victorious lililopo Tabata-Bima jijini Dar es Salaam.

Ninao ujumbe kwa ajili yako na ninaamini kupitia ujumbe huu hasa kipindi hiki tulichomaliza Sikukuu ya Pasaka yenye ujumbe wa ukombozi, utabarikiwa. Kuna mambo mengi yaliyowafunga na yanayoendelea katika maisha ya watu wengi. Pamoja na hayo Mungu anao mpango mzuri na wewe na ana kusudi jema juu ya maisha yako.

Leo nataka tuzungumzie upako wa kukombolewa katika nguvu za giza. Tunapozungumza upako tunamaanisha uwezo, yaani nguvu inayoweza kukutoa kutoka katika nguvu za giza.

Tupo kwenye wakati ambao Yesu Kristo alikufa msalabani kwa ajili yetu ili atukomboe. Imeandikwa katika kitabu cha Wakolosai 1:13 ya kwamba, “Kristo alitukomboa kutoka katika nguvu za giza.”

Watu wengi wanateswa na nguvu za giza zikiwemo za uchawi.

Tukisoma Biblia kwenye kitabu cha Hesabu 24:1, imeandikwa “Basi Balamu alipoona ya kuwa imempendeza Bwana kuwabariki Israel, hakwenda kama hapo kwanza ili kutafuta uchawi bali alielekeza uso wake jangwani.”

Balamu alikuwa ni mtu aliyekuwa anatumika kama mchawi akilaani watu wengi.Kwa hiyo kulikuwa na mfalme anaitwa Balaki alipoona Israel wanakuja hakutaka wale watu wapite kwenye nchi yake.

Kuna watu hawataki ufanikiwe wala ubarikiwe, kwa hiyo alienda kumtafuta mtu atakayewalaani. Sasa hapa tunaambiwa kuwa Balamu alipoona Mungu anataka kuwabariki akafanya hivyo. Katika maisha Mungu anataka kukubariki lakini watu wanaamua kutumia nguvu za giza kukulaani ili waharibu kazi, biashara, familia.

Kwa sababu hiyo Biblia inatuambia safari hii Balaki hakwenda tena kutafuta nguvu ya kuwalaani wana wa Israel.

Katika maisha kuna watu wanatafuta habari zako kwenye nguvu za giza ili kupitia hizo wakumalize. Ila Mungu anao mpango mzuri katika maisha yako na anataka kukusaidia ili akukomboe.

Mungu pekee ndiye anayeweza kuleta mafanikio kwenye maisha yako na ndio maana Nabii Isaya anasema haipaswi watu kutafuta habari zako kwenye nguvu za giza. Unaweza fikiri ni bahati mbaya mambo yako kuharibika, kumbe kuna watu wanaofanya hivyo na Mungu ndiye anayeweza kuyatengeneza na kukukomboa kutoka kwa watu waliosimama kinyume chako. Leo nataka kukuonyesha dalili zitakazokusaidia utambue kama umefungwa na nguvu za giza kama mapepo na unawezaje kujinasua.

Kumbuka Mungu anataka akutoe kwenye hivyo vifungo kwa sababu yeye ni Mungu anayekuwazia mema. Ukiona una dalili kati ya hizo njia pekee ya kutoka ni kumkubali Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako, naye atakufungua.

Dalili ya kwanza ni kuota ndoto kwamba unalishwa au unanyweshwa vitu usingizini. Hii si dalili nzuri na hapo inaonyesha unapewa vitu kwa nguvu za giza.

Pili ni kujikuta umechanjwa chale mwilini. Kuna watu wanapoamka wanaona kuna mikwaruzo au chale fulani mwilini. Kuna mtu alinipigia simu aliota amevamiwa na chui usiku, alipiga kelele na alipoamka akakuta ameparuliwa.

Dalili ya tatu ni kuota unafanya mapenzi na watu au wanyama usiku, nazungumza haya kwa sababu najua wapo watu wanakutana nayo. Jua tu Mungu anakupenda na anakuwazia mazuri, anaweza kukusaidia.

Dalili nyingine itakayokufanya ujue unafuatiliwa na nguvu za giza ni kuota unafanya kazi usiku kama kulima na asubuhi unaamka umechoka. Hii nayo unakuwa unatumikishwa bila wewe kujua.

Pia unaweza kusikia vitu vinatembea kama siafu kwenye mwili wako na hapo jua nguvu za ushirikina zinakufunga.

Kuna wakati unaweza kuhisi ganzi na kichwa kinauma upande mmoja na hakisikii dawa. Yaani unateseka hata kama ukinywa dawa hakiponi jua hali hiyo inahitaji maombi.

Dalili nyingine ni kupoteza kuona darasani. Ukiwa nyumbani unaona na unaweza kusoma vizuri lakini ukifika shuleni huoni hii nayo si dalili njema ambayo Mungu anaweza kukukomboa kwenye tatizo hilo.

Dalili ya nane ni kushindwa tendo la ndoa. Jua kuna mapepo yanayoharibu familia na wakati mwingine unajikuta hupendi mke wako au mume wako. Yaani unaona vibaya kuishi naye, jua Mungu anataka kukuokoa kwenye hilo. Kitu kingine ni kupiga miayo mara kwa mara lakini pia kuhisi unabeba vitu vizito mgongoni.

Hii ni saa yako ya kutoka kwenye hali hiyo mbaya na kumbuka kuna watu wanapenda kuona ukihangaika na kupata tabu.

Lipo jibu la hayo yote. Njia pekee ya kujinasua kutoka kwenye nguvu za giza ni kwa kumfanya Yesu awe mkombozi na mwokozi wako. Mfanye rafiki yako na mkaribishe kwenye maisha yako. Watafute wachungaji ili wakuombee, huna haja ya kuteseka.

Maombi: Baba ninakushukuru, natamka kwa jina la Yesu, roho yoyote inayotenda mabaya, nguvu za ushirikina na kila roho iliyofanya mtu huyu ateseke kuanzia leo naivunja na kuisambaratisha. Natangaza ukombozi, kufunguliwa kwake na kuwekwa huru kwa jina la Yesu. Amen.

Share.

About Author

Leave A Reply