Friday, July 19

UKWELI NDIVYO ULIVYO: Yanga ni kweli ilikosea, ila TFF imekosea zaidi

0


By Badru Kimwaga

HAKUNA siri, Yanga inamhitaji Yusuf Manji, kuliko Manji anavyoitaka Yanga. Ndio, maana Wanayanga wamekubali kuisigiza katiba yao, ilimradi bilionea huyo arejee aendelee na majukumu yake kama mwenyekiti.

Wanayanga wamesamehe kila kitu kama, Manji alitangaza kujiuzulu kwa hiari yake mwenyewe Mei 20 mwaka jana ikiwa ni sawa na zaidi ya siku 500 na ushei.

Manji aliyeingia klabu kama mfadhili tangu mwaka 2006 aliikamata pabaya Yanga kwa kutumia ushawishi wa fedha zake na namna alivyoifanya klabu hiyo kuishi maisha ya kitajiri katikati ya lindi la umaskini. Alitangaza kuachia ngazi, baada ya kuhakikisha klabu hiyo imetetea taji lao la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu mfululizo mbele ya watani zao.

Japo barua yake ilikuja kuanikwa hadharani Mei 23 kama sikosei, lakini Manji alijiuzulu Mei 20, siku ambayo Yanga ilicharazwa bao 1-0 na Mbao katika mechi yao ya mwisho ya kufungia msimu iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Wanachama wa Yanga walitaharuki kutokana na kitendo hicho na kumgomea. Waliandamana kumfuata kwake…Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo nayo walishtushwa wakaitana na kujadiliana na mwishowe kukataa kujiuzulu kwake. Baraza wa Wadhamini la Yanga nao hawakukubaliana na msimamo wa Manji. Wanajua umuhimu wake.

Hata hivyo, kwa kuwa Katiba inaelekeza Mkutano wa Wanachama ndio wenye maamuzi ya kuridhia kujiuzulu kwa viongozi, fasta waliuitisha Juni mwaka jana na kwa kauli moja wanachama walimkatalia katakata Manji kujiuzulu.

Barua ikaandikwa kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambayo nayo Julai 11, mwaka huu iliutangazia umma wameafikiana na msimamo wa Wanayanga Manji bado ni Mwenyekiti halali wa Yanga.

Ikumbukwe uongozi wa kina Manji uliingia madarakani Juni, 2016 hivyo ukomo wake kwa mujibu wa katiba ni mpaka Juni, 2020.

Hata hivyo, tangu alipoangukiwa na kugomewa na wanachama, Manji hakuwahi kuonekana klabuni kwani alipotea kabisa kutokana na mikasa yake na kesi zilizokuwa zikimkabili dhidi ya serikali.

Baadaye alionekana kwenye mechi ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger na kusisitiza atavunja ukimya kwani bado yupo pamoja na Yanga kwa shida na raha. Hakuonekana na kwa mujibu wa Katiba ya Yanga ukomo wa uongozi ni ama kumaliza muda wa kuutumia kwa maana ya miaka minne ama kujiuzulu kwa maandishi na kuwasilisha barua Kamati ya Utendaji.

Pia katika Ibara ya 28 (3) kifungu b ya katiba hiyo ya Yanga mwaka 2010 inasema ukomo wa uongozi ni pale kama hatahudhuria mikutano minne mfululizo ya kawaida ya Kamati Kuu bila ya sababu ya msingi.

Kifungu (c) kinasema iwapo anashindwa utekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo na (d) Anapatikana na kosa la jinai na kuhukumiwa kufungwa bila mbadala wa faini.

Kwa kuangalia baadhi ya vifungu ni wazi, Manji alishakosa sifa, lakini wanachama walishamgomea na TFF ilithibitisha kwa kumtema kwenye Uenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB) Mwenyekiti Clement Sanga kwa kumtambua Manji kama Mwenyekiti.

Msemakweli ni mpenzi wa Mungu, Yanga waliteleza katika ishu nzima ya Manji na kwa mujibu wa Katiba walipaswa kutimisha uchaguzi ndani ya siku 90, lakini siku hizo zilipita kwa vile waliendelea kuamini Manji angerejea klabuni.

Hata hivyo baada ya serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) liliamua kuingilia kati na kuitaka Yanga iitishe uchaguzi kuziba nafasi ya Manji na viongozi wengine waliojizulu akiwamo Sanga na wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.

Kinachoonekana kwa sasa, TFF iliyopewa mamlaka ya kukutana na viongozi wa Yanga ili wajadiliane juu ya uchaguzi huo na kuupangia tarehe ‘wameuteka’ uchaguzi huo, jambo ambalo Wanayanga hawakubaliani nalo.

Yanga wanasisitiza wanataka uchaguzi kama ulivyoitishwa na TFF, lakini kwa nafasi za Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne, huku nafasi ya Uenyekiti isiwepo kwa vile bado wanamtambua Manji kama mwenyekiti wao.

Juzi tu, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Yanga, Kepteni George Mkuchika ambaye ni Waziri wa serikali ya Awamu ya Tano, aliuthibitishia umma kwamba Manji bado ni Mwenyekiti wao kwani kuanzia Desemba 15 atamaliza matibabu na ataanza kuingia ofisini Januari 15, mwakani. Kwa nini TFF imechemka hasa kupitia misimamo ya Kamati yake ya Uchaguzi? Kwanza TFF ilipaswa kujitokeza mapema hadharani na kutengua barua yao ya Julai 11 yenye kumbukumbu Na. TFF/ADM/LM.507/2018 iliyosainiwa na Katibu Mkuu, Wilfred Kidao.

Katika barua hiyo TFF ilikuwa ikiijibu barua ya Yanga yenye kumbukumbu Na. YASC/YMM/002/2018 waliyoandikiwa Juni 12, 2018 juu ya kutambuliwa kwa Manji kama Mwenyekiti Yanga, tena ikikisisitiza kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi ya Wachezaji iliyokutana Julai 11 mwaka huu imeridhia juu ya msimamo wa Yanga.

Kitu gani kilichowabadilisha viongozi hao wa TFF? Hapo ndipo TFF walipochemka na kukosea kuliko walivyokosea wanayanga katika maamuzi juu ya hatma ya Manji ndani ya Yanga. TFF ilipaswa tangu walipoipokea barua ya Yanga kumkana Manji kwa kuamini Yanga imekiuka katiba kwani barua imekuja ikiwa imepita mwaka mmoja tangu Manji alipojiuzulu kwa hiari yake Mei 20, 2017.

Lakini kwa kuwa TFF ilikuwa na dhamira ya kutaka kumweka ‘mtu wao’ ndani ya TPLB, walikubali kumtema Sanga kwa kutangaza hadharani wanamtambua Manji kama Mwenyekiti wa Yanga, lakini wakasahau kuitengua barua yao hiyo ya Julai.

Kadhalika kwa vile TFF ni wasimamizi wa klabu na soka la Tanzania kwa ujumla ni wazi walipaswa kuangalia na kuisimamia Yanga yenye uongozi na Kamati zake ikiwamo ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti Samuel Lukumay, iendeshe mchakato wa uchaguzi wao kama walivyoelekezwa katika barua ya BMT ya Novemba 1, 2018 iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Alex Nkenyenge.

TFF inapaswa kusimamia kuona kama kila kitu kinaenda sawa na pale wakiteleza wangesaidia kurekebisha mambo. Nalisema hili kwa kurejea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Simba ambao ulidaiwa kusitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF enzi ikiwa chini ya Mwenyekiti wake, Revocatus Kuuli kwa madai ya kukiukwa kwa baadhi ya kanuni.

Nini kilichotokea baada ya Kuuli kutoa kauli ya kusitisha uchaguzi huo?

TFF iliingilia kati na Kamati ya Simba iliendelea na mambo yake, huku kukiibuka mzozo mkali baina ya Kuuli na Katibu Mkuu wa TFF, Kidao, kiasi cha mwanasheria huyo (Kuuli) kupelekwa Kamati ya Maadili na kufungiwa maisha hivi karibuni. Kuuli kabla ya kupewa kibano alifunguka mambo mengi kuhusu kilichokuwa kinaendelea ndani ya TFF…kila mdau alimsikia na hata alipoadhibiwa alifunguka pia!

Inawezekana TFF ikaibuka sasa na kudai kesi ya uchaguzi wa Simba haifanani na Yanga, lakini kama wanachama wa Yanga hawajalalamikia juu ya kurejea kwa Manji, kwa nini TFF kupitia Kamati ya Uchaguzi iwapangie wanayanga mambo yao?

Kwa wanaokumbuka hata uchaguzi uliomwingiza Manji na wenzake mwaka 2016 uliingia mzozo kabla ya TFF ya Jamal Malinzi kukubali na kuwaachia Wanayanga wafanye mambo yao wenyewe tofauti na walivyotaka kupangiwa mchakato huo.

Hivyo kwa msimamo huu wa TFF inaweza kuleta picha mbaya mbele ya Wanayanga wakiamini labda kuna kitu nyuma ya pazia kwa masilahi binafsi ya viongozi wake na wanayanga wachache, kuliko masilahi ya Yanga na wanayanga kwa ujumla.

Ndio, maana nadhani Yanga walichemka, lakini TFF inachemka zaidi hata kama ni kweli kinachofanyika ni utekelezaji wa agizo la serikali katika kuhakikisha Yanga inapata viongozi ili kukamilisha safu yao baada ya wenzao kujiuzulu muda mrefu.

Share.

About Author

Leave A Reply