Friday, July 19

‘Ukiukaji haki ndio sababu ya uanaharakati’

0


Swali: Nini kilikusukuma kuingia katika harakati za kutetea haki za binadamu?

Jibu: Kuna vitu ukiviona au kuvisikia vinakusukuma kusema au kufanya kitu. Nilipokuwa nasoma shahada yangu ya uzamili nikiwa kwenye tafiti zangu nilikutana na mambo ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Nikaanza kushangaa watu wanawezaje kufanya vitu kama hivyo.

Lakini, nilipopata kazi katika Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ndipo nilishangazwa na mambo mengi ya watu kufanyiwa vitendo vya ukatili.

Niliwahi kwenda sehemu nikakuta watu wakitoka mnadani polisi wanawakamata na kuwambia wawape pesa zao na watu hao wanajua ndio hivyo. Nilishangaa sana. Nikasema kwa kuwa mimi Mungu amenisaidia nimepata elimu, kuna haja ya kuwasaidia wengine. Nikaona pia kuna haja ya kuonesha kwenye nchi yetu kuna vitu kama hivi pamoja na kuwa nchi inasemekana ni ya amani lakini kuna watu hawana amani ndani ya nchi yao.

Swali: Ni eneo gani la haki za binadamu ulisukumwa zaidi kulisimamia?

Jibu: Kuna mambo mengi lakini kwanza kuna haki za wanawake na watoto ambazo kwenye jamii yetu watu wanaona ni vitu vya kawaida. Mfano, hili suala la watoto wa kike kukeketwa. Kwenye jamii wanaofanya hivyo wanaona ni kitu cha kawaida kabisa. Kuna siku tulienda umasaini kufundisha mambo haya. Mama mmoja akasimama akasema ‘mimi katika maisha yangu nimeshapata maumivu lakini si makali kama siku niliyofanyiwa tohara.’

Sasa huyo mama anatoka kwenye hiyo jamii na ndiye aliyethubutu kusema hivyo, kwa hiyo alitoa mwanya wa kuona kumbe ni vitu vinavyowaumiza hata hao wanaotendewa. Kwa hiyo hilo lilikuwa eneo moja.

Eneo lingine ni pale unapokuta kuna watu kwenye jamii, kwa sababu ya uwezo walionao, wanaweza kuwafanyia wenzao vitu vibaya na mambo yakaisha hivyo.

Utakumbuka pia mwandishi wa habari Adam Mwaibabile (marehemu) alivyobambikiwa kesi na kufungwa mwaka mzima kwa sababu tu ya kutoa taarifa. Kwa hiyo vitu kama hivyo ndio vimekuwa vikinisumbua sana hasa ukiona watu wamepewa mamlaka wa kuwasaidia wananchi badala yake wanatumia mamlaka yao kuwaumiza.

Swali: Unajivunia mafanikio gani ya LHRC chini ya uongozi wako?

Jibu: Kwa kweli mafanikio ni mengi na makubwa. Kwanza tulipoanza hii kazi, hili neno ‘haki’ lilikuwa halifahamiki na hata kama lilifahamika watu walikuwa hawalioanishi na maisha yao.

Kupitia kazi zetu watu wengi wamefahamu na wanazisema haki zao. Kuanzia watoto wadogo hadi watu walio kwenye mamlaka sasa hivi unakuta wanaongelea haki.

Tulipoanza kazi watu wachache sana walikuwa na uthubutu wa kupeleka mashauri yao mahakamani, wengine waliogopa ‘aah! nisije nikalogwa au kufanyiziwa’ lakini baadaye watu wanakuja wengi kwenye vituo vyetu vya msaada wa sheria. Watu wengi sasa wamejua haki zao na wanazifuatilia.

INAENDELEA UK 16

INATOKA UK 15

Mafanikio mengine kubadilisha kwa sheria zinazokiuka haki za binadamu kuwa sheria zinazolinda haki za binadamu. Kuna sheria ambazo zilikuwa hazipo kabisa, kwa mfano, katiba ilikuwa na vipengele vingi sana ambavyo vinakupatia haki halafu vinakunyang’anya. Kuna mabadiliko yalikuja kutokea na kuondoa vipengele karibu vyote hivyo na haki sasa ikawa ni haki timilifu ingawa sasa hivi tuna tatizo jingine, si la kisheria lakini kiutendaji, kwamba mtu una haki lakini inazuiwa na mtu anaweza kusema hiyo si haki na ikawa hivyo.

Hata sheria za ardhi tumefanya kazi kubwa sana ya kujaribu kubadilisha na tumekuja kuwa na sheria nzuri ya haki ya ardhi ambapo hata mwanamke atakuwa na haki ya kumiliki na kutumia ardhi.

Swali: Asasi nyingi za kiraia kama LHRC zinaendeshwa na fedha za wafadhili, utegemezi huu hauwezi kutoa mwanya kwa wafadhili kuwapa ajenda?

Jibu: Kwanza nianze na hilo la pesa. Hivi unajua hizo nchi zinazotoa fedha kwa asasi za kiraia ndizo zinatoa fedha kwa serikali yetu? Na fedha wanatozitoa wao asilimia 75 wanatoa serikalini na asilimia 25 ndio wanatoa kwa asasi zisizo za kiserikali. Kwa hiyo kama wanapenyeza vitu kwa asasi, hata kwa serikali wanafanya hivyo.

Pili, hizo taasisi zisizo za kiserikali zinapata fedha kwa kuzitafuta na kuziomba kwa hayo mashirika. Na hayo mashirika ni wakali sana na fedha zao kiasi ambacho serikali wala hawahitaji kusumbuka kwa sababu wakikosea kidogo tu kwenye mambo ya fedha hawaendelei kupewa.

Ni kweli wanaweza kupenyeza mambo yao usipokuwa mwangalifu. Mie najua kuna vitu fulani walikuwa wanapenda

kuchomekea usipoangalia; masuala ya watu wanaopendana wa jinsia moja wamekuwa wakipenda sana kuchomekea hizo. Lakini ukiwa mwangalifu na ukaona na kuwaambia, hii si sera yetu, hawakulazimishi.

Swali: Inasemekana katika nchi za Afrika ni hatari kuwa ‘kimbelembele’ katika kupambana na mamlaka, umewahi kupata tishio lolote katika utekelezaji wa majukumu yako?

Jibu: Kwa ujumla sijawahi kupokea kitisho kubwa isipokuwa watu wamekuwa wakiniogopesha sana. Tishio moja ambalo halikunitisha ni siku Mkuu wa Wilaya ya Serengeti aliponipigia simu na kuniambia ‘we mama naona umetangaza vita.’ Nikamwambia mheshimiwa nimetangazia wapi vita? Sasa mtu akikwambia hivyo na ni mkubwa, manake na yeye yuko tayari kwa vita.

Kuna siku mtu alinipigia simu, akaniambia, ‘Hivi we mama umewahi kupata tishio?’ Nikamwambia hapana. Baada ya siku mbili nikapata ajali ya gari. Na ile ajali mie niliona ajali tu, lakini sijui kwa nini kila mtu ananiambia haikuwa ajali ya kawaida.

Na unajua siku mbili kabla ya hiyo ajali nilitoka polisi kwenda kufuatilia zile mali zetu zilizokamatwa baada ya Uchaguzi Mkuu, manake nilikuwa nje ya nchi nikarudi baada ya kusikia kompyuta zetu na wafanyakazi wa LHRC wamekamatwa.

Kwa hiyo nikaenda polisi kufuatilia, nimetoka huko ndio jioni nikapata simu, ilikuwa siku ya ijumaa, kwamba ‘we mama hivi umewahi kutishiwa?’ huyo mtu aliyenipigia simfahamu na namba yake iliandika private (binafsi), nikamwambia mi sijawahi kutishiwa, akauuliza hujawahi kutishiwa? Nikamwambia na kwa nini nitishiwe.

Kesho yake Jumamosi, Jumapili nikapata ajali asubuhi.

Swali: Ulijilinda dhidi ya matishio ya uhai na fitina za kisiasa?

Jibu: Kusema kweli sina ujanja, sina mbinu, mimi ni muumini wa dini, Mkristu. Mara nyingi kwa kweli nimekuwa nikimuomba Mungu na huwa naamini ananijibu kwa sababu mimi nilimwambia Mungu hii kazi siifanyi kwa nia ovu, ni kazi kama kazi nyingine, kama nilivyokuwa mwalimu. Sasa hii ndiyo kazi nimeipata, kwa hiyo mimi najikabidhi mikononi kwa Mungu.

Wengine walifikia wakati wakasema waniwekee ulinzi, nikawaambia sidhani kama itasaidia manake mama Gandi aliuawa na mlinzi wake. Kwa hiyo usipomtegemea Mungu hata mlinzi wako au ndugu yako anaweza akatumika akakuua.

Swali: Unaelezeaje hali ya kisiasa na haki za binadamu baada ya kustaafu?

Jibu: Kwa Tanzania tunayoingelea leo, kwa kweli hilo neno haki za kisiasa limekuwa gumu kwa maana hizo haki ziko kisheria lakini zimeminywa kwa kauli za viongozi.

Nakumbuka Rais aliyeko madarakani alipoingia tu alisema tuachane na mambo ya siasa tufanye kazi, na mimi nikafikiri labda anasema kuacha siasa kwa maana ya watu kuongeaongea lakini nikaja kugundua hata vyama vya siasa ambavyo vipo kisheria vinakatazwa kufanya mikutano…Hata hao wanaohama vyama sasa, unasikia mbuge kahama peke yake, hakuna raia hata mmoja aliyemuunga mkono mbuge wake. Nimeona wabunge na madiwani wanahama sijamuona raia anayeenda na hao wabunge.

Na ukiangalia hicho ni kitu kama kimepangwa ndio maana hata barua walizoziandika kwamba wanahama utafikiri ni barua hiyo moja tu manake hata pale palipokosewa kwa barua zote pamekosewa.

Na bahati mbaya mimi naomba niseme kwamba kuna diwani mmoja, sasa hivi ni marehemu, alifika ofisini kwangu na siku nane baadaye aliuawa. Na kitu alichokisema kimojawapo ‘ninashinikizwa nihamie chama cha mapinduzi ili siku Mheshimiwa Rais akija kuzindua daraja niwe mmoja wa madiwani tutakaosema tunamuunga mkono Rais, lakini nimesema sitahama na wameniambia wataniua’. Huyo bwana alicharangwa mapanga hadi kufa. Sasa nikisema hivyo yule ameshakufa na bahati mbaya sikumrekodi lakini mimi kichwani kwangu iko na nilimsikia. Sasa kwa nini nisifikirie hawa wengine labda wana vitisho vinavyowafanya waamue hivyo. Kwa sababu yule bwana aliongea ofisini kwangu, tena tulikuwa tumesimama, akanieleza, na kweli siku nane baadaye huyo bwana amekufa kwa sababu hakuhama chama.

Unadhani mbinu ipi bora zaidi inayoweza kutumika kupunguza matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu kama unavyozielezea?

Mimi ninavyoona na historia inavyojieleza LHRC ni chombo kidogo sana kianachojaribu kuwaonesha watu njia na kufanya kwa kiasi watakachoweza lakini watakaoweza kuleta mabadiliko hapa ni wananchi wa Tanzania pale watakapoona haya mambo hawayawezi tena.

Wao wakiinuka na kuyakataa kwa umoja wao mambo yatabadilika. Nikupe mfano mdogo tu wa kule kigoma. Kuna siku walitaka kumhamisha muuguzi anayeitwa Zai anayefanya kazi yake vizuri sana lakini kwa sababu ya fitina walitaka kumhamisha. Wananchi walilizuia gari lililokuja kuhamisha wakasema haondoki hapa nesi Zai. Hawa walikuwa wananchi wa kawaida tu kule kigoma, na kweli yule nesi hakuhamishwa. Kwa hiyo wananchi wenyewe watakapoona haya mambo hayawafurahishi wao ndio wanaweza kuleta mabadiliko.

Tunafanyaje kama nchi kutoka kwenye hali hii?

Njia nzuri ni kwamba tuendelee kukemea haya mambo lakini pia wananchi waone na kukataa. Wananchi wasipoona na kukataa ni ngumu sana kwa sababu unamshika nani sasa. Kweli hatuna trace? Na zifuatiliwe. Kwa hiyo tusiogope, tusimame na kukemea hivi vitu. Na tusiseme hili ni la hawa, lilianza kwa wanasiasa, likaenda kwa waandishi wa habari, limeendelea kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, wafanyabiashara, mwisho ni kila mtu na si ajabu tukasikia Rais wetu ametekwa, eeh! Manake kama ni watu wasiojulikana utasikia hatumuoni Rais wa Jamhuri, katekwa kwa sababu tunafikiri ni wale wale.

Nini hatma ya Tanzania katika jicho la uzoefu wako kama mwanaharakati wa haki za binadamu?

Mimi napenda sana kuwa chanya, natamani nchi yetu iendelee kuwa nchi nzuri lakini kama tukiendekeza hii hali na watu kuendelea kuwa waoga—na ukiangalia hata kwenye mitandao kuna watu waoga sana, kuna watu wanafiki sana—tukiendelea na hiyo hali tutaiharibu hii nchi. Kwa sababu nchi ya waoga na wanafiki sio nchi, mwisho tutakuja kukuta ndani ya nchi yetu wenyewe tutakuja kupangiwa nyumbani kwetu tule nini na tusile nini kwa sababu tu tumekubali kuachia mambo yaendelee. Bahati nzuri bado kuna watu wanaongea, kuna watu wanatoa tahadhari zikifanyiwa kazi mie nadhani tutaendelea vizuri.

Share.

About Author

Leave A Reply