Saturday, July 20

Uhamiaji yawarudishia hati za kusafiria wanahabari wa CPJ

0


Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji nchini Tanzania imewarudishia hati za kusafiria, waandishi wa habari na wafanyakazi wa Kamati ya Kutetea Waandishi wa Habari Duniani (CPJ), Angela Quintal na Muthoki Mumo baada ya kuzishikilia kwa muda.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Novemba 8, 2018, Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda amesema, hati za kusafiria za wafanyakazi hao, zilishikiliwa kwa muda kwa uchunguzi zaidi.

Amesema tayari wamesharudishiwa kupitia balozi zao na wanaruhusiwa kuendelea kuwepo nchini kwa sababu vibali vyao vinawaruhusu kuwepo nchini hadi Januari 1, 2019

Mtanda amebainisha, kwa kuwa wanahabari hao kama wanataka kuendelea kuwepo nchini wanatakiwa kutekeleza madhumuni ya ujio wao ambayo ni matembezi tu kama walivyoainisha kwenye vibali vyao na hawaruhusiwi kufanya kazi.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC na tumesaini mikataba ya kuondoa viza lakini raia wa nchi hizi wanaruhusiwa kuingia bila viza kwa shughuli za matembezi tu, ila kama wao wanataka kufanya kazi kama walivyokuwa wanafanya mikutano na waandishi wa habari, basi wanatakiwa kuomba vibali kwa mamlaka husika nchini,” alisema Mtanda.

Wafanyakazi hao wa CPJ walikamatwa jana Jumatano na Idara ya Uhamiaji nchini na kushikiliwa kwa muda na baadaye kuachiwa huru kwa tuhuma za kufanya kazi nchini, ikiwemo kufanya mikutano na waandishi wa habari, tofauti na madhumuni ya kufanya matembezi tu ambayo yaliainishwa katika vibali walivyopewa na Uhamiaji wakati wanaingia nchini, kutokea Afrika Kusini na Kenya.

Share.

About Author

Leave A Reply