Saturday, August 24

Ufisadi, kuhonga vyombo vya habari vyamng’oa naibu Kansela Austria

0


Vienna. Naibu Kansela wa Austria amelazimika kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kukabiliwa na kashfa ya ufisadi na kuhonga vyombo vya habari ili vimuandike vizuri.

Kiongozi huyo Heinz-Christian Strache, alinaswa kwenye mkanda wa video ukimuonyesha akihonga mikataba ya biashara ili asiandikwe vibaya katika vyombo vya habari.

Kansela wa Austria Sebastian Kurz amekubali barua ya kujiuzulu ya Strache, baada ya kusambaa ukanda wa video unaomuonesha Strache akihonga mikataba ya serikali ili asiandikwe vibaya katika vyombo vya habari.

Katika taarifa aliyoitoa Jumamosi mchana akiwa ofisini kwake, Strache aliyeonekana kuwa na hasira amesema anajiuzulu ili kuzuia kuanguka kwa muungano unaotawala nchini Austria, lakini aliongeza kwamba amelengwa na kampeni yenye lengo la kuharibu jina na sifa yake.

Chama cha Kurz cha Austrian People’s Party (OVP) kinatawala kwa sasa nchini Austria katika serikali ya muungano na chama cha Strache cha Freedom Party of Austria (FPO). Strache pia amejiuzulu kama mkuu wa chama hicho cha FPO, na kumkabidhi madaraka hayo naibu kiongozi na Waziri wa Usafiri wa Austria Norbert Hofer.

Strache amenaswa kwenye ukanda wa video unaomuonesha akitoa mikataba ya biashara ya serikali kwa mwanamke mmoja tajiri kutoka Urusi, ili amsaidie kukitangaza na kukijengea jina zuri chama chake cha FPO kupitia vyombo vya habari.

Video hiyo iliyonaswa katika kisiwa cha Ibiza nchini Hispania Julai 2017, na kusambazwa Ijumaa jioni, imezua mgogoro ndani ya serikali ya Austria, huku vyama vya upinzani vikidai kuitishwe uchaguzi mpya.

Katika sehemu ya video hiyo iliochapishwa na magazeti ya Ujerumani ya Der Spiegel na Suddeutsche Zeitung, mwanamke anayejiita Alyona Makarova anasikika akimwambia Strache na kiongozi wa kikundi cha bunge cha FPO Johann Gudenus kwamba yeye ni tajiri mkubwa na anataka kumiliki asilimia 50 ya gazeti kubwa la Austria, la Kronen Zeitung.

Kulingana na Suddeutsche Zeitung, mkutano huo ulichukua saa kadhaa, ambapo Strache na Gudenus (wake zao pia wakiwepo) walijadiliana na Makarova jinsi michango ya kifedha isiyo ya moja kwa moja inavyoweza kukisaidia chama hicho kuandikwa vizuri katika vyombo vya habari.

Mkanda huo wa video uliorekodiwa miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa Austria wa Oktoba 2017, ambapo chama cha FPO kilipata asilimia 26 ya kura zote zilizopigwa na kuunda serikali ya muungano na Kansela Kurz.

Makarova amesikika pia akidai kwamba amevutiwa na gazeti hilo ili aweze kukiandikia chama hicho cha FPO kabla ya uchaguzi. Strache na Gudenus walimueleza njia ambazo wafadhili matajiri wanazoweza kuzitumia kuificha michango yao kwa chama cha FPO na moja wapo ni kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali.

Strache alimuambia Makarova iwapo watakubaliana, gazeti la Kronen litaweza kukisaidia pakubwa chama chake cha FPO na kukisogeza mbele katika uchaguzi ili kupata asilimia 34 ya kura badala ya 27. Strache pia alimuahidi njia tofauti za kumlipa mwanamke huyo, ikiwa ni pamoja na kumpatia mikataba ya ujenzi wa miundombinu ambayo kwa sasa inashughulikiwa na kampuni kubwa ya ujenzi Austria ya Strabag.

Wakiyajibu magazeti ya Der Spiegel na Suddeutsche Zeitung baada ya kuchapisha video hiyo, Strache na Gunenus wamesema wakati wa mazungumzo yao walisisitiza “umuhimu wa kuzingatia sheria za Austria,” na kwamba walikuwa wakizungumzia uwezekano wa michango kwa chama cha FPO na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Wanasiasa hao pia wamejitetea kwa kusema kwamba mazungumzo yao yalifanyika katika “mazingira ya starehe na yasiyo rasmi,” na pia kulikuweko na tatizo la kutofahamiana lugha na kwamba hakukuweko mkalimani. Katika video hiyo, Gudenus anasikika akitafsiri Kirusi.

Share.

About Author

Leave A Reply