Friday, August 23

Udahili UDSM wanawake wakitengewa nafasi zao

0


By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Katika mwaka wa fedha 2019/20, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinatarajia kuongeza udahili kwa wanafunzi kutoka 26,460 hadi 28,821 ambalo ni ongezeko la wanafunzi 2,361.

Kati ya hao, wanafunzi wa kike wataongezeka kutoka 10,531 na kufikia 11,584 huku miradi ya utafiti ikiongezeka kutoka 135 hadi 188.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ametoa kauli hiyo bungeni leo Jumatatu Aprili 29, 2019 akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake katika mwaka 2019/20.

Profesa Ndalichako amesema katika kuboresha huduma za kufundisha vyuoni, wizara itawagharamia wanataaluma 112 kuanza masomo ya uzamili lengo likiwa ni kutoa elimu ya kiwango kinachotakiwa.

Amesema katika maboresho makubwa kwa UDSM, wamepanga kuanza ujenzi wa Ndaki ya tiba za afya  na kupanua bweni la John Magufuli kwa ghorofa mbili zaidi na kuendelea na ujenzi katika bweni hilo ambalo linahusisha maduka, saloon, mgahawa na super market.

“Tutakarabati mabweni ya wanafunzi, barabara za ndani na kuanza ujenzi wa jengo la ofisi na vyumba vya madarasa ya shule kuu ya waandishi wa habari na ujenzi wa jengo la taasisi ya sayansi za bahari lililopo Buyuni Zanzibar,” amesema.

Pia, amesema watafanya ukarabati mkubwa wa karakana za uhandisi umeme, uashi, maji na mitambo ambazo zimedumu kwa miaka 40 bila ukarabati na nyumba za walimu wa UDSM kwa gharama ya Sh1.5 bilioni

Share.

About Author

Leave A Reply