Saturday, August 17

Uchunguzi wa DC, muuza madafu kutoleana bastola, panga waendelea

0


By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Blasius Chatanda amesema kwa sababu yupo safarini hafahamu uchunguzi ulipofikia wa sakata la mkuu wa wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali na muuza madafu wanaodaiwa kutoleana silaha.

“Nipo safari nashindwa kuelezea kuhusu uchunguzi, anayekaimu nafasi yangu atakuwa na maelezo zaidi,” amesema Chatanda.

Alipotafutwa kaimu kamanda, Joseph Konyo amesema wamefungua jalada la uchunguzi kupata picha halisi ya tukio lilivyokuwa.

“Tunamtafuta kijana muuza madafu na wananchi waliokuwapo eneo la tukio ili tupate picha halisi ya kilichotokea,” amesema Konyo.

Kauli makamanda hao imekuja siku moja baada ya kuwapo madai kuwa mkuu wa wilaya alinusurika kukatwa panga na muuza madafu.

Machali alipozungumza na Mwananchi kwa simu jana, amesema alisimama kijijini hapo kununua madafu na kuanza kukagua wafanyabiashara ndogo wenye vitambulisho vya ujasiriamali.

Amesema alianza kuwahamasisha wasio navyo wajitokeze, lakini mmoja wa wauza madafu alianza kuikashifu Serikali akisema inawaibia wananchi.

Hata hivyo, Kamanda Chatanda ameshauri mtu anapokuwa na silaha binafsi kwa ajili ya kujilinda awe makini na aangalie anaitoa wakati gani na kwa sababu zipi.

Alisema kama suala lilikuwa ni vitambulisho hakukuwa na haja ya malumbano (kama ikithibitika yalikuwapo kulingana na taarifa zilizopatikana awali), kiongozi hakuna na haja ya kufanya hivyo.

“Kama suala hilo lilionekana la jinai ingetolewa taarifa kwa OCD au kwa watendaji ambao wana jukumu la moja kwa moja kufuatilia suala la vitambulisho vya machinga,    badala ya malumbano,” ameshauri.

Share.

About Author

Leave A Reply