Saturday, August 24

UCHOKOZI WA EDO: Hili la korosho, kuna umuhimu wa kuchutama yaishe

0


By Edo Kumwembe

Juzi nikamsikiliza yule kijana, Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye. Kaongea kwelikweli bungeni. Kaongea haswa. Anasema waliovuruga ununuzi wa korosho kule Kusini mwaka jana ni wahujumu uchumi. Katapika nyongo.

Nilidhani ziara ya Namba Moja kule Kusini ilikuwa imefunga mjadala wa korosho. Nilidhani kila kitu kimeisha, lakini kila siku linaibuka jambo jipya. Kila siku linakuja lingine. Kuna umuhimu wa kuchutama kwa sasa na kuna muda wa kurekebisha mambo.

Mambo madogomadogo ambayo yanaendelea kwa sasa yanatokana na wakosaji kuendelea kuwa viburi. Wangechutama tu halafu tuanzishe mada nyingine. Msimu mwingine wa korosho unakaribia kuwadia kitu cha msingi ni kuhakikisha hatufanyi makosa tena.

Majuzi nilimsikia waziri wa mambo ya korosho amedai kwamba anashangaa kwa nini Watanzania hatuli korosho. Nadhani ni baada ya korosho kubaki maghalani. Umuhimu huu tulifundishwa tangu shule lakini pia tulifundishwa umuhimu wa kuwa na mazao ya biashara. Asilisahau hili. Tukaamua kuuza kuliko kula.

Kauli kama hii ya kufundisha watu umuhimu wa kula korosho inaleta maudhi kwa watu ambao wana korosho zao maghalani. Nadhani ingetoka kauli thabiti ya kumaliza tatizo hili la muda mrefu. Kuna kauli mbili ambazo zingeambatana. Kwanza ni kuhakikisha waliopeleka korosho maghalani wanalipwa. Hili alilisema Namba Moja akiwa ziarani pale Mtwara.

Pia, ingetoka kauli ya kuomba radhi kwa kila kilichoendelea kuhusu korosho. Huwa inatokea kwa waungwana ambao vifua vyao vimejaa uungwana. Pia ingetolewa kauli ya kuthibitisha kwamba msimu huu mambo yataenda sawa.

Msimu mmoja kabla ya msimu huu ambao mambo yameenda hovyo, wakazi wa Kusini walikuwa wanakula raha katika msimu ulio bora pengine kuliko misimu yote katika historia, na ilikuwa katika utawala huu huu.

Sio mbaya kama mambo yameenda hovyo yarekebishwe na neno ‘samahani’ kabla ya kuupokea msimu mwingine na kutofanya makosa tena. Kama kuna siasa zilitumika katika korosho ziwekwe kando. Watu hawataki siasa katika maisha yao ya msingi, kwa uzoefu wangu, korosho ni jambo la msingi kuliko mambo yote kule Kusini.

Share.

About Author

Leave A Reply