Friday, July 19

UCHAMBUZI: Kama Katiba mpya imekwama tusimamie hii ya mwaka 1977

0


Novemba Mosi mwaka huu akiwa katika kongamano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais John Magufuli aliweka bayana kuwa hatatenga fedha kwa ajili ya kuwalipa posho wajumbe kujadili Katiba mpya.

Aliongeza kuwa hata fedha zikipatikana zitapelekwa kwenye miradi ya maendeleo.

Haikuwa mara yake ya kwanza kueleza hivyo kwani amewahi kusema mara kadhaa katika hotuba zake kuwa mabadiliko ya Katiba si kipaumbele chake.

Licha ya kuwa kukamilika kwa Katiba ni miongoni mwa ahadi zilizopo katika ilani ya CCM, Rais Magufuli alienda mbali na kusema kuwa hata watu wanaoguswa kuchangia fedha kwa ajili ya Katiba, wampatie fedha hizo ili afanye shughuli za maendeleo.

Wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa vyama vya siasa na wanasheria wamekuwa wakikosoa msimamo huo wa Rais kwa madai kuwa Katiba ni takwa la wananchi na hata fedha zitakazotumika nazo pia ni za wananchi.

Tumewasikia Jaji Joseph Warioba aliyeongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba na mjumbe wake, Joseph Butiku wakieleza umuhimu wa maoni ya wananchi na umuhimu wa Katiba hiyo.

Wapo pia waliodiriki kusema kuwa ni heri uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwakani na ule Uchaguzi Mkuu wa 2020 nao ukasogezwa mbele kwa muda ilimradi fedha zipatikane lakini yote hayo hayajakubaliwa na Serikali ambayo ndiyo inayopanga matumizi ya fedha na kuamua vipaumbele.

Hoja za wengi zinaonyesha kiu ya watu kupata Katiba mpya na pengine ni matumaini ya wengi kuwa baadhi ya changamoto za kisiasa, kiutawala, uchumi na kijamii zitapata ufumbuzi.

Serikali ambayo ndiyo inayotakiwa kusimamia mchakato huo haijaonyesha nia, lakini Watanzania wanataka kuona mageuzi ya kiutendaji na utawala katika nchi hii kwani si suala la Katiba mpya tu bali matokeo yake ambayo ni mapinduzi ya kiutendaji kwa viongozi na maendeleo ya nchi.

Matakwa haya ya wananchi yanaweza kutekelezwa hata pasipo Katiba mpya bali kwa kuifanyia marekebisho Katiba iliyopo na kuiweka misingi ya kuisimamia ili kila mmoja akajua wajibu na mipaka yake.

Nafikiri kinachotakiwa sasa ni kila Mtanzania kuwa na hulka ya kuheshimu Katiba kuanzia kwa viongozi wa Serikali hata wananchi kwani mapungufu ya Katiba ya sasa si mengi endapo itafuatwa kikamilifu.

Ukiangalia Katiba ya sasa ina vifungu ambavyo vinasimamia utekelezaji wa demokrasia, haki za kijamii utawala wa sheria na maendeleo ya nchi, swali ni je, mapungufu yaliyopo katika maeneo hayo yanatokana na nani?

Jibu ni kwamba kama kuna mapungufu yoyote ni dhahiri kuwa Katiba ya sasa haisimamiwi ipaswavyo au haiheshimiwi kama inavyopaswa.

Mfamo ibara ya 74 ya Katiba yetu ya sasa inaeleza muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi lakini kifungu cha saba cha ibara hiyo kinaonyesha kuwa, “Tume ya Uchaguzi itakuwa ni “idara huru” inayojitegemea, itafanya maamuzi yake rasmi kuhusu utekelezaji wa majukumu yake kwa vikao …”

Hivyo basi inapotokea changamoto yoyote katika Tume ama kwa kuingiliwa na mamlaka nyingine au ikifanya upendeleo wowote, maana yake ni kuwa Katiba haijaheshimiwa.

Endapo kila kiongozi atajua wajibu wake na mipaka yake kwa mujibu wa Katiba ya sasa, huenda kilio cha Katiba mpya kitapungua kwani baadhi ya changamoto zinazozungumziwa zitakuwa zimepata ufumbuzi.

Hitaji la watu si kitabu kipya chenye maneno mazuri kuhusu ustawi wa demokrasia, watu wanahitaji mapinduzi ya kweli na kuona uhalisia wa ustawi katika demokrasia.

Kuna mambo mengi Katiba ya sasa imeyataja vizuri lakini changamoto ipo kwetu sisi wananchi na viongozi wetu waliopewa dhamana kuanzia mamlaka za uteuzi, wateuliwa, Bunge, Mahakama na hata katika vyama vya siasa.

Katiba na sheria vinapaswa kuwa mwongozo wa mambo yote na si kuleta woga, hofu wala vitisho kwa watu wa chini.

Kila mtu afuate sheria inavyoelekeza katika eneo lake na shughuli zake, anayesimamia katiba asionekane kama mchawi kwani uzalendo wa kweli kwa taifa ni pamoja na kuheshimu katiba ya nchini.

Ephrahim Bahemu ni mwandishi wa Mwananchi anapatikana kwa namba- 0756939401

Share.

About Author

Leave A Reply