Sunday, August 25

Ubora wa elimu haupimwi kwa kushusha kiwango cha ufaulu – Askofu

0


By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askofu wa Jimbo Katoliki la Kayanga, Almachius Rweyongeza amesema Tanzania inahitaji elimu bora inayomwezesha mwanafunzi kutatua changamoto za maisha ya kila siku nje ya darasa kwa kuwa na mitalaa iliyofanyiwa utafiti wakina na kujidhihirisha kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Kila mara tunashuhudia mitalaa ya elimu ikibadilishwa mara kwa mara tunasoma si kwaajili ya kupata vyeti,  bali kwa ajili ya maisha na mfumo wa kuwezesha hayo lazima uwe imara la sivyo, baada ya muda mchache  Tanzania itakuwa Taifa  la ajabu,” amesema Askofu Rweyongeza.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Aprili 21, 2019 alipokuwa akihubiri katika Misa Takatifu ya Pasaka iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Mtakatifu George, Jimbo  la Kayanga, Karagwe.

Mhashamu Rweyongeza amesema  vijana wanaoandaliwa kwa gharama kubwa kuwa rasilimali watu, wajenzi wa Taifa, kuhudumu katika viwanda na sekta nyinginezo watajikuta ni vibarua na watumwa katika nchi yao wenyewe.

Amesema Tanzania baada ya kupata uhuru, muasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius  Nyerere alibainisha maadui watatu ambao ni  ujinga, maradhi na umasikini hivyo baada ya kumshinda mkoloni akaona kazi bado kuna kazi ya kufanya.

“Lakini tujiulize ni rasilimali au mbinu gani Taifa limeweza kupambana na adui ujinga na maradhi ili kupata amani na maendeleo ya kweli?,” amehoji.

“Kwenye  geti la chuo kikuu fulani kuna maandishi yaliandikwa ‘Ukitaka kuangamiza taifa lolote huhitaji kutumia silaha ya nyuklia, njia nzuri ya kuangamiza ni kuharibu mfumo wa elimu.

Aliendelea kunukuu maandishi hayo  yaliyosema ‘Ruhusu mbumbu waonekane wamefaulu na wasonge mbele hadi vyuo vikuu, matokeo yake yatajidhihirisha baada ya muda. Mbumbu hao wakishahitimu kwa kupata vyeti feki, wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari na manesi, majengo yataporomoka mikononi mwa wahandisi, pesa zitapotea mikononi mwa wachumi na mafisadi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa dini na serikali kuchezea elimu ni kuchezea amani na Taifa.

“Kwanza je, mfumo wetu wa elimu ni kama biashara au ni haki elimu bila watu, kubadilishwa kwa sera na miongozo ya elimu si ishara kwamba Watanzania hatujui nini tunachotaka, rasilimali watu wawe na sifa gani na hatujui tunataka taifa letu la leo na kesho liweje,” amesema

Amesema Ubora wa elimu haupimwi kwa kulegeza viwango vya ufaulu ili kuongeza idadi ya washindi badala yake inaongeza upele na majipu yanayotumbuliwa na Rais John Magufuli kila kukicha.

“Tuendelee kumuombea Rais wetu wa awamu ya tano kwa ujasiri wa kuendelea kupambana na maovu ambayo yaliota mizizi katika nyanja mbalimbali za utumishi wa umma,” ameongaza.

Share.

About Author

Leave A Reply