Thursday, August 22

Tuhuma za utapeli kwa kutumia laini 629 za simu zampandisha kizimbani

0


By Hadija Jumanne na Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkazi wa Bungu A, Fadhil Mahenge (27) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kutakatisha fedha kiasi cha Sh123 milioni kwa kutumia laini za simu 629 za mitandao tofauti.

Mahenge ambaye ni mfanyabiashara kwa njia mtandao (Online Busness) anakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la  kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa njia ya udanganyifu.

Fadhil ambaye ni miongoni mwa ‘Wazee wa Ile Pesa tuma kwenye Namba Hii’ amesomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu  Mkazi, Wanjah Hamza.

Wakili wa Serikali Batilda Mushi akisaidia na Costantine Kakula amedai leo Alhamisi Aprili 18, 2019 kuwa mshtakiwa anakabiliwa wa kesi ya uhujumu uchumi namba 31/2019.

Mushi amedai katika shtaka la  kwanza, ambalo ni kusambaza taarifa za uongo, mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 2017 na Machi 2019 katika jiji la  Dar es Salaam, Rukwa na Songwe pamoja na maeneo mengi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Anadaiwa kusambaza ujumbe yenye maneno ya tuma pesa  kwenye namba hii.

Pia siku na maeneo hayo, Mahenge anadaiwa kusambaza ujumbe mfupi wa maneno katika simu za mkononi bila ridhaa ya mtumiaji wa simu husika kwa kutumia line za simu  629 za mitandao tofauti.

Katika shtaka la  tatu, siku na maeneo hayo, mshtakiwa anadaiwa  kusambaza ujumbe bila ridhaa ya mpokeaji kwa nia ya kujipatia fedha.

Mushi amedai katika shtaka la nne, mshtakiwa anadaiwa kwa makusudi alijipatia  fedha kiasi cha Sh123milioni kwa watu tofauti kupitia laini za simu 629.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo katika kipindi hicho na maeneo hayo, Mahenge anadaiwa kutakatisha fedha haramu kiasi cha Sh123 milioni, wakati akijua  kuwa fedha hizo ni zao la kosa la  kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa kesi hiyo haina dhamana na Mahakama hiyo haina mamlaka ya kumpatia dhamana isipokuwa Mahakama Kuu pekee.

Mushi amedai upelelezi wa kesi haujakamilika, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Hamza ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 2, 2019 itakapotajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande.

Katika hatua nyingine, wafanyabiashara wawili ambao ni wakazi wa Kigamboni wamepandishwa mahakamani hapo kujibu shtaka la kuchapisha habari katika mtando bila kuwa na leseni.

Washitakiwa hao ni Obadia Kwitega na Stella Ommary ambao wamesomewa shtaka lao  na  Wakili wa Serikali, Constantine Kakula mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwezile.

Wakili Kakula alidai kuwa washitakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 29 na Machi 29, 2019 katika maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam ambapo kupitia runinga ya mtandaoni ikijulikana kama Habari Mpya TV walichapisha taarifa bila kibali cha Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Washtakiwa baada ya kusomewa mashitaka hayo, walikana kutenda kosa hilo.

Wakili Kakula alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Rwezile alitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao ambapo kila mshtakiwa anatakiwa kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini dhamana ya maneno ya Sh5milioni.

Pia kila mshtakiwa anatakiwa kusaini dhamana ya maneno ya  Sh5milioni.

Hata hivyo, mshitakiwa Stella ndiye aliyeweza kutimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana, huku mwenzie akirudishwa rumande.

Hakimu Hamza aliahirisha kesi hiyo hadi  Aprili 30, 2019, itakapotajwa.

Share.

About Author

Leave A Reply