Tuesday, August 20

TTB yajivunia watalii kutoka Israel

0


By Filbert Rweyemamu,Mwananchi [email protected]

Arusha. Idadi ya watalii kutoka  nchi ya Israel imeongezeka  nchini hatua inayoifanya kutoka nchi ya 20 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hadi kuwa nchi ya sita kwa kiwango cha watalii wanaotembelea vivutio vya utalii ndani ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Devotha Mdachi ameliambia Mwananchi kuwa kuongezeka kwa watalii hao ni kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia na hatua ya hivi karibuni ya Tanzania kufungua ubalozi nchini humo.

Amesema idadi ya watalii kutoka Israel kuja nchini kwa mwaka ni 40,000 kiwango ambacho kimeongezeka kwa kipindi kifupi na kuipa matumaini bodi hiyo kuona umuhimu wa kuliona taifa hilo kama mdau maalumu wa kukuza uchumi kupitia mapato ya utalii.

“Naomba ifahamike kuwa April 20 mwaka huu tulipokea watalii 1,000 kutoka Israel hii ni mara ya kwanza kwa wakati mmoja ndege nne kubwa kuleta idadi hiyo kwa wakati mmoja ndio maa na Waziri Mkuu aliona kuna sababu ya kuja kuzungumza nao na kuwaaga ili wawe mabalozi wa utalii kwa nchi yetu,” amesema Mdachi.

Ameongeza kuwa watalii wa Israel wanapenda kutalii nchi zenye amani na utulivu kuangalia wanyamapori, utamaduni, fukwe za bahari pamoja na kutembelea mambo ya kale kujifunza mambo mbalimbali.

Ametaja nchi 10 zinazoongoza kwa idadi ya watalii kuja nchini zikiongozwa na Marekani, Uingereza, Ujerumani, Italia, India, Israel, Ufaransa, China, Uholanzi na Canada .

Jumamosi Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa ,Waziri wa Maliasili na Utalii,Hamis Kigwangalla, mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na viongozi wengine walishiriki tukio muhimu la kutambua uwepo wa siku saba wa watalii hao nchini.

Mmoja wa watalii kutoka Israel ambaye ni mwanadiplomasia nchini Bulgaria anayehusika na uchumi, Alon Cohen amesema wamefurahishwa na hali ya uoto wa asili ulivyo pamoja na utulivu nchini na kuahidi kuendelea kupanga safari za kuja kutalii.

“Ujumbe ninaowapa Waisrael kote duniani nawaambia waje Afrika hasa Tanzania kuna mambo mengi ya kuja kuona ,wapo watu wazuri na wanaokaribisha wageni, pia ni sehemu ya kuchangia uchumi wa nchi hii,” amesema Cohen.

Pia mtalii Josef Agas ambaye ni mara yake ya kwanza kutembelea nchini amesema alifika maeneo mbalimbali yakiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Hifadhi ya Taifa ya Manyara na maeneo mengine ambayo yamemvutia sana.

Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Excellent Guides Tanzania, Samson Kyashama ambayo ilikua miongoni mwa waliopokea watalii hao, amesema wanaishukuru TTB na Serikali kuandaa safari ya makampuni madogo kwenda Israel mwezi wa Februari mwaka huu kutafuta masoko.

Amesema safari hiyo imeleta matokeo chanya ya kupata watalii na anatarajia kabla ya mwaka huu kuisha kampuni yake itaendelea kupata watalii zaidi kutoka Israel kutokana na ushirikiano uliopo katika kampuni yake na mawakala wa utalii nchini humo.

Share.

About Author

Leave A Reply