Friday, August 23

TLS yaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwaonya Ma RC, DC

0


By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetoa pongezi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, George Mkuchika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi kwa hatua yao ya kukemea vitendo vya wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka watu mahabusu bila sababu za msingi.

Onyo hilo la Waziri Mkuchika lilitolewa Aprili 15, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake ya mwaka 2019/2020.

Barua ya pongezi iliyotolewa jana Alhamisi Aprili 18, 2019 na Rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala ilisema wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao na kukiuka taratibu za kisheria.

“Kwa niaba ya baraza la uongozi la TLS napenda kuipongeza Serikali hususani Waziri (Mkuchika) pamoja na kuwepo kwa mwongozo wa kisheria, TLS inampongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa waraka na kuusambaza kwa wahusika wote kama ilivyonukuliwa toka kwenye majibu ya Waziri,” anasema Dk Nshala.

Dk Nshala anasema wito wa TLS kwa Mwanasheria Mkuu ni kumtaka kuusambaza waraka huo kwa vyombo vya habari na wananchi ili wananchi wote waufahamu na waweze kuhoji pale madaraka yanapotumika vibaya.

“Kwa muda mrefu sana TLS na wanachama wake wamesikitishwa sana na mwenendo huo wa baadhi ya wakuu wa mikoa, wilaya na hata baadhi wa watumishi wa Serikali hususani Jeshi la Polisi kwa kutumia madaraka yao vibaya na kuwaweka kizuizini wananchi na mawakili kinyume na utaratibu uliowekwa na sheria,” anasema Dk Nshala.

Anasema vitendo hivyo ni uvunjwaji wa Katiba na Sheria za nchi kwani havitokani na mtu au wakili kuwa ametenda kosa bali kwa lengo la kuwakomoa, kuwatisha, na kujikuza hivyo TLS haina budi kuipongeza Serikali kwa kuwakumbusha viongozi kuheshimu misingi ya katiba.

Dk Nshala ambaye amechaguliwa kuongoza jumuiya hiyo hivi karibuni, anasema TLS inathamini uhusiano bora na taasisi zote za Serikali lakini haitasita kuwataka wanachama wake na wananchi kuwashitaki viongozi wa Serikali wanaokiuka sheria ikiwa ni pamoja na kuwaweka ndani mawakili na wananchi ambao hawajafanya kosa lolote lile la jinai wala kuhatarisha amani.

“Katiba ya nchi yetu inatoa hakikisho la watu kuwa huru na kuwa uhuru huo tu unaweza kuingiliwa pale mtu anapokuwa ametenda kosa la jinai na si vinginevyo. Utawala wa sheria unadai kufuatwa kwa sheria na watu wote ikiwemo viongozi wote wa Serikali,” anasema.

Anasema viongozi na polisi ndio wanaotakiwa kuwa mfano wa kufuata sheria. Kufuatwa kwa sheria hujenga imani kwa Serikali, mahakama na Bunge na huchagiza utawala bora ikiambatana na ustawi wa nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa. “Ubabe huondoa imani ya wananchi kwa Serikali, mahakama, na Bunge lao.

Anasema mahakama ndiyo mhimili pekee wenye mamlaka ya kuamua migogoro baina ya watu au watu na Serikali si wakuu wa mikoa au wa wilaya, hivyo kesi zipelekwe mahakamani kwa kuwa ndicho chombo chenye kauli ya mwisho juu ya kesi hizo na si kiongozi yeyote yule wa Serikali.

Share.

About Author

Leave A Reply