Thursday, August 22

Terminal III JNIA sasa kukabidhiwa Mei

0


By Rosemary Mirondo [email protected]

Dar es Salaam. Serikali imesema ujenzi wa jengo jipya (Terminal III) la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), limekamilika na mwezi ujao litakabidhiwa.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele alipozungumza na gazeti hili jana. Alisema ujenzi umekamilika kwa asilimia 96 na kilichobaki ni umaliziaji mdogo.

“Tunatarajia kazi zote zitakamilika Mei kama ilivyopangwa awali likiwa na miundombinu yote muhimu ya umeme na mingineyo pamoja na maduka ambayo yapo kwenye hatua za mwisho za kukaribisha wawekezaji,” alisema.

Ujenzi wa jengo hilo ulitarajiwa kukamilika Desemba 2017 lakini ukasogezwa mbele kwa mwaka mmoja, halafu ukasogezwa tena hadi Mei 2019.

Likiwa na viwango vyote vya kimataifa, Kamwele alisema kutokana na takwimu zilizopo jengo hilo litaelemewa muda mfupi ujao hivyo mipango inaandaliwa kukabiliana na hali hiyo.

“Tulianza na Terminal I yenye uwezo wa kuhudumia abiria 500,000 kwa mwaka, kisha Terminal II inayomudu abiria milioni 1.5 kabla hatujajenga hii ya tatu itakayohudumia abiria milioni sita,” alisema.

Baada ya kuzidiwa, alisema Terminal I iliachwa kwa ajili ya kuhudumia viongozi na ndege ndogo za kukodi wakati Terminal II ikiwa kwa ajili ya wasafiri wa ndani na kimataifa. Mwaka jana pekee, Kamwele alisema Terminal II ilipokea zaidi ya abiria milioni 2.6 wa ndani na milioni 3.8 wa kimataifa hivyo kuwa na jumla ya abiria milioni 6.4. Ongezeko hilo, alisema limewapa ishara kuwa kitu cha ziada kinapaswa kufanywa haraka kuboresha huduma hiyo inayokua kila siku.

Alisema ndani ya miaka miwili tangu jengo hilo litakapozinduliwa, Serikali itatafuta eneo jingine mjini Bagamoyo ili kujenga uwanja mbadala au kuutumia wa Dodoma kwa ajili ya abiria wa kimataifa.

Jengo hilo lililojengwa na kampuni ya BAM International BV ya Uholanzi na kusimamiwa na Arab Consulting Engineers ya Misri, ujenzi wake umegharimu Euro 254 milioni (Sh560 bilioni).

Share.

About Author

Leave A Reply