Sunday, August 18

Tanzania yafunikwa kila kona Afcon U17

0


By Thobias Sebastian

KABLA ya kuanza kwa mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17), ambayo jana Jumatano yalichezwa nusu fainali, baadhi ya nyota wa timu ya vijana wa umri huo ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ walitabiriwa kutamba lakini mambo yakawa sivyo.

Faida ya kucheza nyumbani na viwango bora walivyoonyesha kwenye mashindano mbalimbali ambayo Serengeti Boys walishiriki, ilitoa tumaini kwamba wachezaji kama Kelvin John ‘Mbappe’, nahodha Morice Abraham, Edmund John na wengineo wangekuwa tishio kwenye fainali hizo.

Hata hivyo hilo halikutimia kwa Mbappe na wenzake na kujikuta wakiaga mapema katika hatua ya makundi baada ya kufungwa mechi zote tatu dhidi ya Nigeria, Uganda na Angola.

Kana kwamba haitoshi nyota hao wa Serengeti Boys wameondoka patupu kwani wameshindwa kutwaa hata tuzo ya mchezaji bora wa mechi ambayo hutolewa kwa kila mchezaji anayefanya vizuri kwenye kila mchezo wa mashindano hayo.

Mechi ya ufunguzi ilikuwa Tanzania dhidi ya Nigeria tuzo ya mchezaji bora ilikwenda kwa Akunmi Amoo wa Nigeria, mchezo wa pili Angola na Uganda tuzo ilikwenda kwa Osvaldo Capemba.

Mechi ya Cameroon na Guinea na tuzo ilikwenda kwa Steve Mvoue, Senegal na Morocco ilikwenda kwa Tawfiq Bentayeb, wakati mechi ya pili ya wenyeji Tanzania dhidi ya Uganda na tuzo ilikwenda kwa Mganda Ivan Asaba.

Mchezo wa raundi ya pili wa kundi A baina ya Nigeria na Angola tuzo ilikwenda kwa Mnaigeria Tijani Thrilled, huku kule kwenye kundi B, mechi ya Cameroon na Morocco tuzo ilikwenda kwa Saidou Ismaila na mwingine wa Guinea na Senegal ilikwenda kwa kipa Sekou Camara wa Guinea.

Tanzania ilicheza mechi ya mwisho na Angola na tuzo ilikwenda kwa Zito Luvumbo kutoka Angola, wakati mchezo wa pili kati ya Uganda na Nigeria tuzo ilikwenda kwa Ibraheem Jabaar, huku mechi za makundi zikiitimishwa na mechi mbili kati ya Cameroon na Senegal ambayo mchezaji bora alikuwa Ismaila Saidou,wakati Morocco na Guinea ilikwenda kwa kipa wa Morocco Taha Mourid.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema si kwamba wachezaji wa Serengeti Boys hawakucheza vizuri na hawakustahili kupata tuzo ya mchezaji bora bali matokeo ambayo waliyapata kufungwa katika kila mchezo ni miongoni mwa kigezo ambacho kilichangia kuwanyima.

“Ukiangalia kama Mbappe alikuwa ancheza vizuri ila katika timu alionekana yupo mwenyewe huku timu pinzani kuna kama yeye si chini ya wachezaji watatu kwahiyo wenzake walionekana kuwa bora na wakisaidina kuzipa timu zao matokeo mazuri na kuweza kuchukua tuzo hizo,” alisema Pawasa.

Katika fainali za AFCON U17 zilizofanyika Gabon, mshambuliaji Abdul Seleman ambaye kwa sasa anachezea Simba, aliitoa kimasomaso Tanzania kwa kupata tuzo hiyo kwenye mchezo dhidi ya Angola ambao Serengeti Boys iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Share.

About Author

Leave A Reply