Wednesday, August 21

Tanzania, Kenya kudhibiti magonjwa ya mlipuko

0


By Filbert Rweyemamu, Mwananchi [email protected]

Arusha. Nchi za Tanzania na Kenya ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinatarajiwa kufanya tukio la mfano la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yanayovuka mipaka (cross borders) kwenye mpaka wa Namanga unaotenganisha nchi hizo mbili.

Tukio hilo linalofanyika leo Jumanne  Mei 21, 2019 ni maandalizi ya tukio kamili litakalofanyika Juni 11 hadi 14 mwaka huu eneo hilo la wilaya ya Longido upande wa Tanzania na Kajiado upande wa Kenya na litahudhuriwa na wataalamu kutoka nchi zote za EAC.

Taarifa ya EAC iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema eneo la EAC limeshuhudia matukio ya magonjwa ya kuambikizwa yakivuka mpaka kutoka nchi moja mwanachama kwenda nyingine na yamekua yakiathiri afya za binadamu na wanyama.

Magonjwa hayo ni Ebola, kichaa cha mbwa, homa ya bonde la ufa, kipindupindu, polio na tauni na kuwa magonjwa hayo si kwamba yanaathiri afya za binadamu na wanyama pekee bali pia yanaathiri shughuli za kilimo, biashara, utalii na mazingira kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na mkuu wa mawasiliano kwa umma wa sekretariati ya EAC, Richard Owora iliongeza kuwa jumuiya hiyo inalenga kuwa na utaratibu wa afya kwa pamoja (one health approach) utakaosaidia kupunguza athari za magonjwa hayo.

Uratibu huo wa kudhibiti magonjwa ya mlipuko unaratibiwa na EAC kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo  la Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kupitia mradi wa Utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (PanPrep).

Share.

About Author

Leave A Reply