Saturday, August 24

Tambwe, Kamusoko wavunja ukimya Yanga

0


By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Wachezaji nyota wa kigeni wa Yanga, Amissi Tambwe na Thabani Kamusoko, wamezungumzia hatma zao ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Tambwe alisema ataikumbuka Yanga kwa namna ilivyompokea baada ya kutemwa na Simba msimu Desemba, 2015.

Nyota huyo alisema baada ya kuachwa na Simba alikuwa katika kipindi kigumu, lakini Yanga ilimuokoa kwa kumpa ajira.

Tambwe alisema Yanga ilithamini mchango wake tangu siku ya kwanza na hawezi kuisahau hata kama atakuwemo katika mipango ya kocha Mwinyi Zahera.

Kauli ya Tambwe na Kamusoko, zimekuja baada ya kuibuka taarifa kuwa hawataongezwa mkataba kwa ajili ya msimu ujao, baada ya mikataba yao kumalizika.

“Sijazungumza na uongozi kuongeza mkataba mpya, lakini nimepokea ofa nyingi hata nikiondoka Yanga, popote nitakapokuwa nitaikumbuka timu hii.

“Nilipotoka Simba, Yanga ilinipokea vizuri imenilea kisoka, mashabiki, wachezaji na viongozi walinipa ushirikiano mkubwa nitaikumbuka hata ikitokea nimeondoka Yanga,” alisema Tambwe.

Kamusoko nahodha wa zamani wa Platnum ya Zimbabwe, alisema ataendelea kuiheshimu Yanga kwa kuwa wasifu wake katika soka umechangiwa na Yanga.

“Nimejiunga na Yanga nikiwa sijawahi kupata taji hata moja la ligi japo nilikuwa na nafasi ya kucheza katika timu kubwa na nilikuwa na uwezo, hivyo kitu pekee ambacho nitakuwa nakikumbuka Tanzania ni historia niliyoweka na upendo wa mashabiki na viongozi,”alisema Kamusoko.

Zahera alisema wachezaji wa kigeni walikuwa na msaada msimu huu akiwamo Tambwe ambaye alisema licha ya kuanzia benchi, amekuwa akifanya vyema.

Hata hivyo, Zahera alisema Tambwe na Kamusoko bado ni wachezaji wa Yanga na uamuzi wa kutangaza majina ya wachezaji watakaotemwa atatangaza majina baada ya kumalizika mechi yao na Azam kesho.


Share.

About Author

Leave A Reply