Saturday, July 20

Sugu apagawisha wabunge akivalia suti, King naye kumbe wamo

0


Dodoma. Ama kweli usisafirie nyota ya mwenzako, kwani ukifanya hivyo unaweza kupishana na matokeo yake iwe shida kwako. Hongera Sugu umetisha umeliteka jukwaa.

Ni mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye leo Jumatano Novemba 7, 2018 ameamua kurudi katika enzi hizo huku akivamiwa jukwaani kama malkia wa nyuki anavyozungukwa kwa ajili ya ulinzi.

Jamaa amepanda jukwaani katika uzinduzi wa mkakati wa mpango kujumuisha masuala ya jinsia ndani ya Bunge uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa jijini Dodoma ambapo ukumbi mzima umebadilika na kuwa sehemu ya burudani kwa dakika chache.

Ilikuwa ni kama sinema kwani alipanda jukwaani ikiwa imepita saa moja tangu alipotaka kukinukisha ndani ya ukumbi wa Bunge alipotaja masuala ya mauaji na kupimwa akili kwa wabunge na viongozi wa juu wakati wa mchango wake kuhusu mpango wa taifa.

Katika mchango wake ndani ya Bunge, amezungumzia ugumu wa maisha huku akimmwagia sifa Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kwamba aliwasaidia watu wengi akiwemo yeye aliyetokea mtaani tu lakini hadi akajikuta yuko mjengoni.

Lakini muda mfupi baadaye amepanda jukwaani alipoitwa akiwa ni mbunge wa kwanza katika tamasha hilo fupi lililojaa mvuto wa kila aina yake na akajizolea fedha za kutosha kutoka kwa wabunge walionyosha mikono kumtunza.

Mara alipoitwa na kupewa kipaza sauti, alionekana kama mtu aliyebadilika ghafla kutoka uheshimiwa na kuingia katika usanii huku akiwa amevalia suti yake nadhifu ikiwa ni tofauti na wasanii wengi ambao huwa wanapanda majukwaani.

“Watu wote piga makofiiiiiii…piga makofi ha hiiii unajua lazima kuchangamka,” amesikika Sugu ambaye alipiga kibao cha chini ya miaka 18 huku akiwakaribisha kwenye tamasha lake siku ya Jumamosi Novemba 10 jijini humo.

Wimbo huo uliwapagawisha si wabunge pekee bali hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi kwenye halfa hiyo, pamoja na kutabasamu lakini alianza kutikisa kichwa akiashiria kwenda na ‘biti’ huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akiangua kicheko pamoja na Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai.

Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta aliongoza kundi la wabunge kwenda kumtuza Sugu ambaye aliimba kwa ufupi lakini kelele zilisikika zikimtaka kuendelea na katika miondoko yake ya kufokafoka.

Wabunge wengi walisimama na kuanza kucheza huku mikono ikiwa juu wakimpungia na baadhi walitaka asishuke katika jukwaa. Ni kibao chake cha zamani ambacho alikiimba kwa umahiri ingawa tofauti ni kwamba enzi hizo alikuwa akipiga ‘jeans’ na fulana au shati ambalo halijachomekewa lakini safari hii amepanda jukwaani akuimba akiwa amepiga suti na tai.

Mbunge mwingine ambaye naye alionyesha kuwavutia wabunge wengi alikuwa ni Mbunge wa Jang’ombe (CCM) Ally Hassan ‘King’ ambaye alipagawisha kwa kuimba taarabu kwa ufupi kwenye tamasha hilo lakini idadi ya washangaliaji ilikuwa ni kubwa.

Mapema leo asubuhi Sugu alizungumza na Mwananchi akasema mikakati yake kuwa anataka kurudi kwa nguvu kwenye majukwaa na kwamba atafanya matamasha mengi mfululizo.

Share.

About Author

Leave A Reply